Habari Mseto

Ojaamong akana kwenda Ujerumani kuponda raha

July 16th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Busia Sospeter Ojaamong, Jumatano alikiri mbele ya mahakama kwamba alizuru Ujerumani lakini akakanusha alienda kuponda raha.

Ojaamong, ambaye alianza kujitetea katika kesi ya ufisadi wa Sh8 milioni inayomkabili, alimweleza Hakimu Mkuu Douglas Ogoti kwamba aliandamana katika ziara hiyo na madiwani, waziri wa masuala ya mazingira na maafisa wengine wakuu wa serikali yake.

Wakati wa ziara hiyo, alisema, walizuru maeneo mengi nchini Ujerumani kujionea jinsi uzoaji taka unavyosimamiwa.

Kwenye ziara hiyo, alisema, waliandamana pia na wanahabari waliopeperusha ziara hiyo kutoka Ujerumani hadi humu nchini.

“Baada ya kuzuru Ujerumani, mimi na maafisa wakuu wa kaunti tulitia sahini mkataba wa maelewano (MoU) na kampuni ya Ujerumani ya Madam-R Enterprises. Kampuni hiyo ingeshughulikia uzoaji taka katika kaunti yangu ya Busia,” akasema Ojaamong.

Alikanusha madai ya polisi kwamba yeye na msafara wake walienda Ujerumani kustarehe.

“Ziara yangu ya Ujerumani haikuwa ya kujistarehesha, wala haikuwa ya kula njama za kufilisi Kaunti ya Busia. Ilikuwa ya kujifahamisha jinsi aina mbalimbali za taka zinavyoweza kugeuzwa kuwa za manufaa kwa wakazi wa Busia,” alisema Ojaamong.

Ojaamong aliomba mahakama itupilie mbali mashtaka yanayomkabili.

Bw Ojamong ameshtakiwa pamoja na Bernard Yaite, Allan Ekweny na waziri wa fedha Samuel Ombui.

Washtakiwa wengine ni Timon Otieno, Leonard Wanda, kampuni ya Madam R Enterprises na wakurugenzi wake Edna Adhiambo, Renish Achieng na Sebastian Hallensleben, raia wa Ujerumani.

Washtakiwa wanaendelea kujitetea.