OKA hatarini kusambaratika vinara wakimenyania tiketi ya urais

OKA hatarini kusambaratika vinara wakimenyania tiketi ya urais

Na SHABAN MAKOKHA

Mzozo unanukia katika One Kenya Alliance (OKA), kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi wakipigania tiketi ya mgombea urais wa muungano huo kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Haya yanajiri huku Bw Musyoka akisisitiza kuwa atakuwa kwenye debe katika uchaguzi huo na washirika wa Bw Mudavadi wakiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala wakishikilia kuwa ni sharti kiongozi huyo wa ANC ateuliwe kugombea urais wa OKA.

Akizungumza katika boma la mwaniaji wa kiti cha udiwani cha wadi ya Mayoni, eneobunge la Matungu, Anerico Maero, Bw Malala alidokeza OKA itaisha iwapo Mudavadi hatateuliwa mgombea urais wake.

OKA unaoleta pamoja Mudavadi, Kalonzo, Moses Wetangula (Ford Kenya) na Gideon Moi(KANU) haujasajiliwa kama muungano wa kisiasa. Mnamo Ijumaa, Mudavadi alisusia mkutano wa vinara wa OKA uliotarajiwa kutangaza mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti kushindana na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Bw Wetangula, Bw Musyoka na Bw Moi walilazimika kuahirisha tangazo hilo,

Lakini Jumamosi, Bw Musyoka, katika mkutano alioitisha nyumbani kwake Yatta, kaunti ya Machakos, alisisitiza kuwa atakuwa kwenye uchaguzi wa urais kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Bw Malala alidai kwamba Bw Mudavadi ana wafuasi wengi kuliko Bw Musyoka na ilikuwa makosa kwa kamati ya kiufundi ya OKA kumteua kiongozi huyo wa Wiper kupeperusha bendera ya muungano huo uliopendekezwa.

Aidha alidai kwamba Bw Mudavadi aliunga Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kwenye chaguzi zilizopita na wawili hao wanafaa kurudisha mkono kwa kuunga Bw Mudavadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Mwaka wa 2007, Mudavadi alikubali Kalonzo kuwa makamu rais na Raila kuwa waziri mkuu. Mwaka wa 2013, aliacha azima yake ya urais na kuwa meneja wa kampeni za Bw Odinga. Sasa ni wakati wa hao wawili kurudisha mkono. Tutabaki katika OKA iwapo Mudavadi akuwa mgombea urais wa muungano huo kwenye uchaguzi mkuu ujao,” alisisitiza Bw Malala.

Nao viongozi wanaounga KANU na Azimio la Umoja eneo la Magharibi wanataka Bw Moi kujiondoa OKA wakidai kushindwa kwa vinara kutaja mgombea urais wao kunatatiza azima yake.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli alimtaka Bw Moi kuondoa KANU kutoka OKA akisema hatakubali kuwa nje ya serikali ijayo.

Akizungumza akiwa shule ya wasichana ya Khwisero mnamo Jumamosi, Bw Atwoli alisema Kanu imekuwa sehemu ya serikali zilizopita tangu uhuru na Bw Moi hafai kukubali kuelekeza wanachama katika upinzani.

“Anafaa kuondoka OKA haraka au nitaitisha mkutano wa wabunge wote wa Kanu na kuwaondoa OKA. Niko tayari kutumia uwezo wangu kuhakikisha Kanu itaingia katika Azimio la Umoja kwa kuwa ndiyo itaunda serikali,” alisema Bw Atwoli.

  • Tags

You can share this post!

Sngura wa siasa wasiojua baridi

Mvutano kuhusu fidia kikwazo kwa mradi wa Sh36 bilioni Pwani

T L