Michezo

Oktay asema uwanja wa Afraha ulizuia Gor kufuma mabao mengi

February 18th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Gor Mahia, Hassan Oktay ameutaja uwanja wa Afraha mjini Nakuru ulioandaa mechi yao ya ligi dhidi ya Sofapaka Jumapili Februari 17, 2019 kama ‘shamba’ kutokana na hali mbovu ya uwanja huo.

Hata baada ya kuwatandika Batoto ba Mungu 1-0 , bao lililofungwa na Samuel Onyango, Oktay amesema kwamba haingekuwa ubovu wa uwanja wa Afraha, K’Ogalo wangeshinda mechi hiyo kwa idadi ya juu ya mabao.

“Nafurahishwa na namna wanasoka wangu walivyocheza soka. Lakini inasikitisha kwamba ligi ya KPL iko katika mwaka wake wa 10 ilhali uwanja wa kuchezea bado unakaa hivi. Nakiri kwamba leo tumecheza katika shamba,” akasema Oktay.

Raia huyo wa Uturuki vile vile alilalamikia mrundiko wa mechi za kuwajibikia akisema umeanza kuathiri wachezaji wake walionekana kulemewa na uchovu.

“Ratiba hii inachosha na kuchisha kwasababu tumecheza mechi nyingi kwa kipindi kifupi. Sijawahi kuzungumza kuhusu marefa lakini wa leo alifanya maamuzi mengi mabaya yasiyofaa.

Ni mtindo mbaya kwasababu walitudhulumu wakati wa Debi ya Mashemeji na katika mechi zilizopita kwa kuyakataa mabao tuliyoyafunga wakisema washambulizi wetu waliotea,” akaongeza Oktay baada ya kuichapa Sofapaka.

Hata hivyo, Oktay alikiri kwamba walikuwa na presha ya kutwaa ushindi baada ya nambari mbili Mathare United kutoshana nguvu na Zoo Kericho, matokeo ambayo yaliwapa msukomo wa kupata ushindi ili kupungaza mianya kati K’Ogalo na timu za Bandari FC na Mathare United walioko mbele yao kwenye msimamo wa jedwali la KPL.

Gor wana nafasi murwa ya kushikilia uongozi wa KPL kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2018/19 iwapo watapata ushindi dhidi ya Western Stima mnamo Jumatano.