Michezo

Okumu achezeshwa mechi nzima Elfsborg ikipiga Ostersunds 1-0

August 13th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BEKI Mkenya Joseph Okumu alichezeshwa mechi nzima timu yake ya Elfsborg ikitia kapuni alama tatu baada ya kulemea wenyeji Ostersunds 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Soka Uswidi, Agosti 9.

Elfsborg, ambayo inarejea uwanjani leo Alhamisi dhidi ya Falkenberg, ilinunua Okumu mnamo Agosti 2019 kwa kandarasi ya miaka mitatu kutoka Real Monarchs nchini Amerika.

Hapo Agosti 9, Elfsborg ilipata goli la ushindi kutoka kwa Jesper Karlsson dakika ya 50. Karlsson alisukuma kiki kali hadi wavuni baada ya kupokea kona murwa iliyochanjwa na Johan Larsson.

Timu ya Elfsborg ilimaliza mechi hiyo ya raundi ya 14 wachezaji 10 baada ya Simon Strand kulishwa kadi nyekundu dakika ya 63.

Katika mchuano mwingine, beki wa pembeni kushoto Eric Ouma Otieno almaarufu Marcelo alikosa mechi yake ya 15 mfululizo timu yake ya AIK ikipondwa 3-1 na wenyeji Mjallby uwanjani Strandvallen.

Mshambuliaji wa Nigeria Moses Ogbu aliweka Mjallby kifua mbele dakika ya 10 kabla ya kiungo wa Ghana Enoch Adu kusawazisha dakika 29 baadaye kupitia penalti.

Hata hivyo, AIK, ambayo iliajiri Ouma hapo Januari 1, 2020 kwa kandarasi itakayokatika Desemba 2024, ilienda mapumzikoni mabao 2-1 chini baada ya Ogbu kufungia Mjallby bao la pili kupitia penalti dakika ya 43.

Mambo yaliharibikia AIK zaidi pale kinda Taylor Silverholt aliongezea Mjallby bao la tatu dakika ya 76. Marcelo, ambaye ni mmoja wa wachezaji muhimu katika timu ya taifa ya Kenya, anaendelea na mazoezi kujiandaa kurejea ulingoni baada ya kuumia mwezi Mei mwisho mazoezini.

Kwenye jedwali, Malmo inaongoza kwa alama 31 baada ya kushinda mechi yake ya saba mfululizo ilipozaba Falkenbergs 1-0 mapema Jumapili. Elfsborg inafuata katika nafasi ya pili kwa alama 27. Imeruka Norrkoping, ambayo itamenyana na wavuta-mkia Helsingborg katika mechi yao ya 14 mnamo Jumatatu usiku.

Norrkoping imezoa alama 25, huku klabu ya zamani ya mshambuliaji wa Kenya Michael Olunga, Djurgarden ikifuata katika nafasi ya nne kwa alama 23. Mjallby ni ya saba kwa alama 19, nayo AIK inapatikana katika nafasi ya 12 kwa alama 13 baada ya kuambulia alama mbili kutoka mechi sita zilizopita.

Aidha, Jonkopings Sodra anayochezea mshambuliaji wa kati Mkenya Erick Johana Omondi iliimarisha rekodi yake ya kutoshindwa kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Uswidi ilipokung’uta Umea 1-0 Agosti 8. Jonkopings, ambayo inashikilia nafasi ya nne kwenye ligi hiyo ya timu 16, ilipumzisha Omondi sekunde chache baada ya muda wa kawaida kumalizika na kujaza nafasi yake na raia wa Ghana Enock Kwakwa.