Okumu arejea kikosini Gent ligini Ubelgiji, Kapaito aokoa Arbaminch Ethiopia

Okumu arejea kikosini Gent ligini Ubelgiji, Kapaito aokoa Arbaminch Ethiopia

Na GEOFFREY ANENE

BEKI Joseph Okumu alirejea kikosini baada ya mechi moja nje na kusaidia timu yake ya KAA Gent kuduwaza Standard Liege 3-1 kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji ugani Ghelamco Arena, Jumapili.

Mshambuliaji Tarik Tissoudali kutoka Uholanzi alifungia Gent bao katika dakika ya 22 na 67. Gent pia ilinufaika na bao la kujifunga kutoka kwa beki wa Liege, Hugo Siquet, dakika ya 57.

Goli la Liege kufuta machozi lilipatikana kupitia kiungo Aron Donnum dakika ya 69. Ushindi huo ulikuwa wa nne mfululizo wa Gent dhidi ya wageni Liege ugani Ghelamco.

Gent inakamata nafasi ya saba kwa alama 24 baada ya kujibwaga uwanjani mara 16 kwenye ligi hiyo ya klabu 18. Iko alama mbili nje ya mduara wa kufuzu kushiriki Klabu Bingwa Ulaya.

Nchini Ethiopia, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita Eric Kapaito alifungia washiriki wapya Arbaminch bao la kusawazisha 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi Fasil Kenema kupitia penalti dakika ya 74 ugani Hawassa University.

Arbaminch ilikuwa imepoteza penalti kutoka kwa Abebe dakika ya saba kabla ya Fasil kuchukua uongozi kupitia penalti mapema katika kipindi cha pili wakati Ashenafi alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea Bereket Desta visivyo ndani ya kisanduku.

Fasil ilikamilisha mechi watu tisa baada ya Yared Bayeh na Habtamu Takese kulishwa kadi nyekundu. Beki Mkenya Benard Ochieng’ pia alikuwa katika kikosi cha Arbaminch dakika zote 90.

Fasil inaongoza ligi hiyo ya klabu 16 kwa alama 10 nayo Arbaminch ni ya tatu pointi mbili nyuma baada ya michuano mitano.

You can share this post!

Kibarua cha Raila waasi wakirejea ODM

Real Madrid yacharaza Sevilla na kufungua mwanya wa pointi...

T L