Na GEOFFREY ANENE
MWANATENISI Angella Okutoyi alianza mashindano ya chipukizi ya daraja ya pili ya Shirikisho la Tenisi Duniani (ITF) ya J2 Al-Solaimaneyah kwa kubwaga Roisin Gilheany kwa seti 2-1 nchini Misri hapo Agosti 30.
Okutoyi, ambaye atamenyana na Mbelgiji Juliette Bovy katika raundi ya pili baadaye Agosti 31, ni msichana pekee Mkenya anayeorodheshwa ndani ya wachezaji 1,400-bora duniani katika nafasi ya 188.
Alimlemea Gilheany (392 duniani) kutoka Australia kwa alama 3-6, 7-6, 6-4 katika raundi ya kwanza naye Bovy akamlemea Mmisri Mariam Ibrahim 6-1, 6-2.
Okutoyi anashiriki mashindano yake ya tatu mfululizo jijini Cairo. Alikamilisha mashindano ya kwanza ya daraja ya tatu J3 Cairo katika hatua ya robo-fainali (Agosti 16-20) na kufika nusu-fainali katika mashindano ya pili ya J3 Cairo (Agosti 23-27).
Akimbwaga Bovy, Okutoyi atapepetana katika robo-fainali na mshindi wa mechi kati ya Mtunisia Feryel Be Hasen na raia wa Urusi Maria Sholokhova.