Okutoyi apigwa breki raundi ya pili tenisi ya Nottingham Uingereza

Okutoyi apigwa breki raundi ya pili tenisi ya Nottingham Uingereza

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Angella Okutoyi mnamo Jumatano alibanduliwa katika raundi ya pili kwenye mashindano ya tenisi ya J1 Nottingham nchini Uingereza.

Okutoyi, ambaye anakamata nafasi ya 61 kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Tenisi Duniani (ITF), amepoteza dhidi ya Mturuki Aysegul Mert (nambari 64) kwa seti 2-0 za 7-5, 7-6(12).

Bingwa huyo wa zamani wa Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 alikuwa ameanza kampeni vyema Juni 21. Alipepeta nambari 340 duniani Given Roach kutoka Uingereza 7-5, 6-4 katika raundi ya kwanza.

Okutoyi, ambaye ameshiriki mashindano ya kifahari ya chipukizi ya Australian Open na French Open mwaka huu, anajiandaa pia kwa mashindano ya haiba ya Wimbledon yatakayofanyika nchini Uingereza mnamo Julai 2-10.

Aidha, Jumatano imekuwa siku mbaya kwa Wakenya kwenye mashindano ya Afrika ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 14 yanayoendelea jijini Cairo, Misri. Ayush Bhandari, Baraka Ominde, Stacy Yego na Melissa Mwakha wamepoteza kwa seti mbili bila jibu dhidi ya Omar Hossam (Misri), Yassin Ahmed (Misri), Milla Kotze (Afrika Kusini) na Morgan Jordaan (Afrika Kusini) mtawalia. Ominde na Brian Nyakundi walishirikiana katika mechi ya wachezaji wawili kila upande wakipoteza 6-3, 6-0 dhidi ya Wamisri Omar Hossam na Eyad Reda.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa Simba United apongeza vijana wake kwa kufaulu...

Rais Kenyatta akataa kutia saini mswada wa kuumiza...

T L