Michezo

Okutoyi na Nkatha wazidi kuipa Kenya matumaini katika tenisi Afrika

August 25th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WANATENISI Angella Okutoyi na Judith Nkatha ndio wamesalia kupeperusha bendera ya Kenya katika fani hii kwenye michezo ya Afrika (African Games) katika kitengo cha kinadada cha mchezaji mmoja kwa mmoja jijini Rabat nchini Morocco.

Katika mechi zilizosakatwa Agosti 24, Okutoyi alibwaga raia wa Ivory Coast Marie Biansumbra kwa seti 2-0 za alama 6-2, 6-3 naye Nkatha alinufaika na Mzimbabwe Valerie Bhunu kujiuzulu. Hata hivyo, mambo yalikuwa magumu kwa Alicia Owegi alipolimwa 2-0 (6-2, 6-1) na raia wa Madagascar Sariaka Radilofe naye Faith Omurunga akanyolewa na wembe huo na Deandra Osabuohien (Nigeria) kwa alama 6-2, 6-0.

Kenya pia ilikuwa na matokeo mseto katika tenisi ya wanaume hapo Jumamosi pale Albert Njogu alilambisha sakafu Bernard Alipoe-Tchotchodji (Togo) kwa seti 2-0 (6-4, 6-0) naye Ismael Changawa akaonyeshwa kivumbi na Mmoroko Mohamed Dougaz 2-0 (6-4, 6-0).

Baada ya kubwaga Mamadouba Makadji (Guinea) 2-0 Agosti 23, Kevin Cheruiyot alirejea uwanjani Jumapili kwa mechi za raundi ya 16-bora na kupoteza kwa seti 2-1 dhidi ya Sabry Sherif kutoka Morocco.

Ibrahim Kibet aliondolewa mashindanoni baada ya kulazwa na Mzimbabwe Takanyi Garanganga 2-0 Ijumaa. Njogu ameratibiwa kukabiliana na Christian Saidi Otopio kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baadaye Jumapili katika mechi ya raundi ya 16-bora.

Okutoyi na Nkatha watarejea uwanjani Agosti 28 kwa mechi za mchezaji mmoja kwa mmoja dhidi ya Salma Ziouti wa Morocco na Barakat Oyinlomo kutoka Nigeria, mtawalia.