Michezo

Ole Gunnar ajiandaa kuiadhibu Man City

April 23rd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Manchester United Ole Gunnar Solskajaer anaamini kwa debi kati yao na majirani Manchester City Jumatano ni jukwaa bora la kujifufua baada ya kichapo kikali mikononi mwa Everton.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) walipokezwa kipigo cha aibu cha 4-0 na Everton Jumapili Aprili 21 ugani Goodison Park na kudidimiza zaidi matumaini yao ya kutinga nne bora mwishoni mwa msimu wa 2018/19.

“Mechi itakayotukutanisha na Man City ndiyo kubwa zaidi tuliyosalia nayo. Wachezaji wangu wameathirika sana kisaikolojia baada ya kichapo cha Everton na niliandaa mkutano nao ili kuwapa motisha kwamba wanaweza kubadilisha hali kwa kuichapa Man city kwenye debi,” akasema Ole Gunnar.

Mkufunzi huyo ambayo wachanganuzi wanaendelea kutilia shaka uwezo wake wa kuingoza Man United kufikia ufanisi kama zamani hata hivyo amewataka mashabiki kuwapa vijana wake sapoti ili wapate motisha ya kutosha kuwakabili wapinzani wao kiume.

“Natumai mashabiki watakuwa kiungo muhimu kwenye jitihada zetu za kuilaza Man City ugani Old Trafford. Kwa kweli wachezaji wetu wanajua waliwavunja moyo mashabiki lakini hawafai kuhukumiwa kwa kuwa hii ni soka na matokeo ya kuridhisha huwa hayapatikani kila mara. Ni jukumu langu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuwafurahisha mashabiki wetu,” akaongeza Ole Gunnar.

Mechi hiyo ni muhimu kwa timu hizo mbili kwa kuwa ushindi utawawezesha Man City kupaa hadi kileleni mwa ligi. Man U nao watafufua uwezo wao wa kumaliza miongoni mwa timu nne kwenye EPL iwapo wataondoka na ushindi katika uga wao wa Old Trafford.