Michezo

Ole Gunnar asema lengo kwa sasa ni kushinda mechi 5 kati ya 6 zilizobaki

April 3rd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema nafuu pekee kwa timu hiyo ni kushinda mechi tano kati ya sita zilizosalia ili kumaliza ndani ya klabu nne bora.

Man United walipata pigo kuu katika juhudi zao za kutinga nne bora pale walipochabangwa 2-1 na Wolvehampton Jumanne Machi 2 kwenye mechi kali ya Ligi Kuu ya Uingereza(EPL).

United walichukua uongozi kupitia Scott MCTominay kabla ya Diogo Jota kuwasawazishia wenyeji. Beki Chris Smalling alijifunga mwenyewe na kuipa Wolveshampton bao la ushindi baada ya beki mwenza Ashley Young kutimuliwa uwanjani kwa kupokezwa kadi nyekundu.

Hata hivyo Ole Gunnar alisikitikia timu yake kukosa kutumia nafasi nyingi za wazi, hali ambayo ingewapa ushindi na kutoa upinzani mkali kwa timu zinazowania nafasi nne za kwanza EPL ikielekea ukingoni.

“Tungetumia nafasi zetu vizuri tungeimarisha nafasi yetu ya kutinga nne bora. Tulikuwa tunahitaji alama 18 baada ya mechi za kimataifa kukamilika katika mechi nane zilizosalia. Tulipata alama tatu dhidi ya Watford na sasa tunahitaji alama nyingine 15 ili tusiwe na mwanya mkubwa wa kupoteza mechi nyingi na kukosa kutimiza lengo letu,” akasema Ole Gunnar.