Michezo

Ole Gunnar asema Pogba haendi Real, alilenga kumfurahisha Zidane

April 1st, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amekanusha kuwa nyota wa klabu hiyo Paul Pogba analenga kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

Wakati wa kipindi kifupi cha mapumziko kwa ajili ya mechi za kimataifa, Pogba alinukuliwa akisema angefurahi sana kutimiza ndoto ya kucheza chini ya kocha mpya wa Real Madrid Zinedine Zidane ambaye pia nia raia mwenzake Ufaransa.

“Jinsi nimewahi kusema, ni ndoto ya kila mchezaji kuchezea Real Madrid ambayo ni mojawapo ya klabu kubwa zaidi duniani. Pia wana Zinedine kama kocha wao na ni ndoto ya kila mchezaji kufundishwa soka na jagina huyo aliyetamba sana enzi zake akiwa mwanasoka,” akasema Pogba.

Kuzidisha tetesi kwamba Pogba yuko njiani kuelekea uwanja wa Santiago Bernabeu, kocha wa huyo wa Real Madrid alisema alimjibu Pogba kwa kusema anatamani sana kuwajibisha raia mwenzake uwanjani akivalia jezi ya Real Madrid.

Hata hivyo Ole Gunnar akizungumzia kabla ya mtanange wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) dhidi ya Wolves Jumanne Aprili 2 alisema Pogba anafurahia maisha ndani ya Old Trafford na matamshi yake yalilenga tu kufurahisha Zidane.

“Ingawa sipendi kuzungumzia timu nyingine, ni wazi kwetu kwamba Pogba anayafurahikia maisha ya hapa na alikuwa akijibu swali akiwa na nia ya kufurahisha raia wa taifa lake. Bado ana nafasi hapa na ningependa kujenga himaya ya timu hii kwa kumtumia. Hakuna kilichobadilika na kivyovyote vile ataendelea kusalia hapa,” akasema Solskjaer.