Michezo

Ole Gunnar sasa aitaka Man U iwasajili Messi na Ronaldo

April 17th, 2019 1 min read

MASHIRIKA NA JOHN ASHIHUNDU

MANCHESTER

Kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United sasa anataka klabu yake ifanye juhudi kuwasajili mastaa Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Juventus.

Raia huyo wa Norway amesema yuko tayari kufanya nao kazi pale Old Trafford iwapo watakubalia kujiunga na miamba hao majira ya kiangazi.

“Iwapo watakubali kuagana na klabu zao za sasa na kutua Old Trafford nitawapokea kwa mikono miwili kwa sababu ni wachezaji wazuri zaidi,” alisema Solskjaer.

Hata hivyo, wengi wameona maoni ya kocha huyo kuwa ya kushangaza kwa vile sio rahisi kwa wawili hao kuondoka waliko sasa.

Kocha huyo alisema hayo baada ya kutangaza mipango yake ya kukisuka upya kikosi chake baada ya kupewa miaka mitatu kujaza nafasi ya Jose Mourinho.

Solskjaer ambaye amepewa fedha za usajili ametangaza mpango wa kuwatimua wachezaji kadhaa wa Man-U akiwemo nahodha, Antonio Valencia, kufuatia vichapo vitatu tangu apewe kazi hiyo.