Michezo

Ole Gunnar Solskjaer anavyowapa motisha 'Mashetani Wekundu'

February 4th, 2019 2 min read

NA JOB MOKAYA

KOCHA wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameleta mabadiliko mengi timuni. Muhimu kwa yote ni kwamba timu inashambulia. Man-United chini ya kocha wa zamani Sir Alex Ferguson ilikuwa na mazoea ya kushambulia.

Mazoea hayo yalianza kufifia tangu Ferguson aondoke na mtindo wa kushambulia kuzikwa kabisa katika kaburi la sahau chini ya Jose Mourinho almaarufu ‘The Special One’ ambaye aliacha kuwa ‘Special’ kabisa.

Kabla ya ujio wa Ole, ‘Mashetani Wekundu’ walikuwa kama timu ndogo ya mtaani iliyojihamu na kushambulia kwa kushtukiza.?Matokeo mema nayo yaliadimika kama yai la jogoo sikwambii maziwa ya fahali.

Nani amewahi kunywa maziwa ya fahali? Vivyo hivyo matokeo duni yalifanya mtu kupigwa kalamu na mwingine kuingia.

Binafsi nilikuwa nimeacha kutazama mechi za Man-United kwa sababu ziliudhi sana.?Tangu kupewa nafasi ya kuongoza majuma saba yaliyopita, Solskjaer ameleta ushindi wa nane mfululizo na kuwa kocha wa kwanza kufanya hivyo katika historia ndefu ya timu hiyo.?Kwa kocha mstaafu Sir Alex Ferguson, ilimchukua mechi 18 kupata ushindi wa nane.

Katika kipindi ambacho kocha huyu kutoka Norway amekuwa uongozini, hakuna timu nyingine katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambayo imepata pointi 19, kufunga zaidi ya mabao 19, kuwa na mikwaju zaidi ya 130 kutengeneza nafasi za ufungaji zaidi ya 95?na kufungwa mabao machache sana.

Majarida mengi ya habari nchini Uingereza na hata mataifa mengine yamesheheni habari za namna kiungo Paul Pogba alivyoimarika chini ya Solskjaer ila Pogba siye mchezaji wa pekee aliyeimarika chini ya kocha huyu msimamizi.

Washambulizi wote wa Man-United wamevamia eneo la adui mara nyingi zaidi baada ya kila dakika chini ya kocha huyu. Kwa mintaarafu hii, Marcus Rashford ndiye aliyenufaika zaidi kwa kupewa nafasi ya kucheza kwenye nambari tisa.

Rashford ameanza mechi katika nafasi hii zaidi ya mara sita na kufunga zaidi ya mara tano ndani ya mechi hizi. Kijana huyu mwenye umri wa miaka 21 anafurahia maisha mapya chini ya kocha mpya.?Naye Paul Pogba amefunga zaidi ya mabao 11 msimu huu katika mechi zote.

Tayari huu ndio msimu ambapo Pogba amefunga mabao mengi zaidi katika taaluma yake ya uchezaji soka.?Akiwa Juventus, msimu ambapo Pogba alifunga mabao mengi zaidi ulikuwa kati ya 2014 na 2016 ambapo alifuma nyavu mara 10 katika misimu hiyo. Pogba mwenyewe amebadilika sana chini ya kocha huyu na inavyoonekana, maisha yake ni?mazuri zaidi ugani Old Trafford.

Chini ya Solskjaer, Pogba hufunga au hutoa krosi nyingi zinazosababisha ufungaji wa mabao kwa kila dakika 72. Tangu Solskjaer kupewa majukumu ya kuongoza, Pogba amechangia magoli mengi zaidi ligini zaidi ya mchezaji yeyote katika soka ya bara Ulaya.