Habari

Ole Sapit amkataza Riggy kutoa nafasi kwa wabunge kuongea kanisani, Nyahururu


ASKOFU Mkuu wa Kanisa La Kianglikana Nchini Jackson Ole Sapit Jumapili, Juni 23, 2024 alikataa ombi la Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba mbunge mmoja ahutubie waumini katika Kanisa hilo mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia.

Fursa ya kipekee ambayo Bw Gachagua alipewa ni ile ya kusoma majina ya takriban wabunge 20 waliofika hapo kuhudhuria hafla ya kutawazwa kwa Askofu mpya Samso Mburu, kunena machache kisha kumwalika Rais William Ruto.

“Idadi  ya waheshima wabunge waliofika kuungana nasi katika hafla hii ni kubwa mno. Kwa hivyo, Askofu Mkuu naomba nimpe mmoja wao nafasi kidogo ya kusalimia watu wa Mungu,” Bw Gachagua akamuomba Ole Sapit.

“Haya, sawa nitaheshimu uamuzi wako Baba Askofu Mkuu,” Bw Gachagua akasema, ishara ya kusalimu amri baada ya Askofu huyo Mkuu kukatalia mbali ombi lake.

Baadaye, Naibu Rais alijikita katika masuala ya kuwahimiza waumini kudumisha umoja huku akitoa wito kwa viongozi kutekeleza majukumu yao, kabla ya kumwalika Rais Ruto.

Askofu Ole Sapit alionekana kuitikia wito wa vijana wa Gen-Z wanaopinga Mswada wa Fedha wa 2024 kwamba wanasiasa wazimwe kuongea makanisa Jumapili ya Juni 23, 2023.