Habari

Ole wao walioficha mamilioni

June 2nd, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU na BENSON MATHEKA

SERIKALI imechukua hatua ya kukabiliana na watu walioficha manyumbani mwao pesa wanazopata kupitia ufisadi na ulanguzi wa fedha kwa kufutilia mbali noti za Sh1,000 na kuanzisha noti mpya.

Jumamosi, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Patrick Njoroge alisema noti zote za Sh1,000 zilizokuwa zikitumika zinapaswa kubadilishwa na zile mpya kufikia Oktoba 1.

“CBK imemaliza kutengeneza noti za sura mpya kuambatana na Katiba na sheria zote husika. Noti hizo zilitolewa Ijumaa kupitia kwa tangazo rasmi na sasa ni pesa halali,” alisema Dkt Njoroge.

Hii inamaanisha kwamba watakaokosa kubadilisha pesa hizo kufikia tarehe hiyo hawataweza kuzitumia mahali popote kwa sababu zitakuwa haramu.

Dkt Njoroge alitoa tangazo hilo Rais Uhuru Kenyatta alipozindua noti mpya za sarafu mbalimbali punde tu baada ya kuongoza taifa kuadhimisha Siku ya 56 ya Madaraka katika Kaunti ya Narok.

Hii ni kumaanisha kuwa wananchi watakaokuwa na noti hizo katika nyumba zao baada ya tarehe hiyo hawatakuwa na uwezo wa kuzitumia kwa sababu hazitakuwa halali.

Kulingana na gavana huyo, noti za Sh1,000 zimekuwa zikitumiwa na watu laghai wanaotengeza pesa feki ambao huhofia kuzipeleka katika benki wakihofia kuchunguzwa na asasi husika za serikali. Kuficha pesa majumbani kadhalika hupunguza kusambaa kwa pesa miongoni mwa wananchi na hivyo kutatiza biashara, uwekezaji na hata ustawi wa taifa.

“Hivi majuzi tumeona noti ghushi nchini, hali hiyo imezua hofu kubwa kwani inaweza kutatiza matumizi ya fedha na katika biashara. Ili kukabiliana na hali hiyo kabisa, noti zote za zamani za Sh1, 000 zitaondolewa sokoni kufikia Oktoba 1. Wananchi wanastahili kuzibadilisha kwa sababu baada ya siku hiyo hazitakuwa halali,” alisema.

Alifafanua kuwa kabla ya tarehe hiyo, noti hizo zitatumiwa pamoja na zile mpya zilizozinduliwa jana.

Litakuwa pigo kubwa kwa wananchi wanaoficha pesa nyingi manyumbani, hasa wafanyabiashara, wananasiasa, na walaghai kwa sababu itakuwa vigumu kubadilisha viwango vikubwa vya fedha.

Kulingana na sheria za Benki Kuu ya Kenya, mwananchi yeyote anayechukua au kuweka zaidi ya Sh1 milioni katika benki, huwa anahitajika kujaza fomu maalum kuelezea zilikotoka pesa hizo au anakozipeleka, anayelipa au kulipwa na kusudi lake.

Mabunda

Katika vita vya kukabiliana na ufisadi vinavyoendelea nchini na ambavyo Rais Kenyatta aliapa kutolegeza kamba, baadhi ya watu wamekuwa wakipatikana wakihifadhi mabunda ya pesa katika nyumba zao.

Rais Uhuru Kenyatta atoa hotuba ya Madaraka Dei Juni 1, 2019, Narok, Kenya. Picha/ PSCU

Mapema mwaka 2019, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai George Kinoti alisema washukiwa wa ufisadi wameficha pesa katika nyumba zao.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa michango mikubwa katika harambee na kuzua maswali kuhusu wanakotoa pesa hizo.

Noti zote kuanzia kwa sarafu ya Sh50, Sh100, Sh200, Sh500 na Sh1,000 zitakuwa na picha ya Jumba la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta (KICC) na picha za nyati, chui, simba, kifaru na ndovu.

Kila noti inatoa wazo fulani, kwa mfano, noti ya Sh50 inatoa wazo la nishati hai, Sh100 (kilimo), Sh200 (huduma kwa jamii), Sh500 (utalii) na Sh1,000 (usimamizi).

Noti za zamani za Sh50, Sh100, Sh200, Sh500 hazitaondolewa na zitaendelea kutumiwa pamoja na zile mpya. “Itakuwa rahisi kwa vipofu kutumia noti hizo,” alisema Dkt Njoroge na kuongeza kuwa CBK itahamasisha wananchi kuhusiana na sifa za noti mpya.

Dkt Njoroge alisema noti mpya ni salama maradufu zikilinganishwa na noti za awali.