Michezo

Oliech ajumuishwa katika kikosi cha Gor Mahia michuano ya CAF

August 7th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MVAMIZI matata wa zamani wa Harambee Stars, Dennis Oliech amejumuishwa katika kikosi cha Gor Mahia kitakachonogesha kampeni za kuwania ufalme wa Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League) msimu huu.

Oliech aliyekosa sehemu kubwa ya kampeni za Gor Mahia mwishoni mwa msimu uliopita, anatarajiwa kushirikiana vilivyo na sajili wapya watakaoongoza safu ya uvamizi ya Gor Mahia.

Baada ya kuagana na nyota Francis Kahata, Jacques Tuyisenge, Harun Shakava na Francis Mustafa, Gor Mahia wamejishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu.

Jitihada zao zimewawezesha kujinasia maarifa ya masogora watatu wa kigeni ambao wanatarajiwa kuwavunia Gor Mahia mabao muhimu yatakayowapigisha hatua zaidi katika kivumbi cha CAF msimu huu. Watatu hao ni Dickson Ambundo, Gislain Yikpe Gnamien, na Francis Afriyie waliosajiliwa kutoka Tanzania, Ivory Coast na Ghana mtawalia.

Chipukizi Eliud Lokuwom, Erick Ombija na Kennedy Otieno aliyesajiliwa kutoka Western Stima muhula huu wameachwa nje ya kikosi hicho cha Gor Mahia. Sogora mwingine ambaye ametemwa na Gor Mahia kwa minajili ya kivumbi hicho cha kimataifa ni kiungo Hashim Sempala ambaye yuko pua na mdomo kuagana na miamba hao waliomsajili kutoka Tusker msimu uliopita.

Kocha msaidizi Patrick Odhiambo anatazamiwa kuongoza Gor Mahia dhidi ya Aigle Noir ya Burundi katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Agosti 11 jijini Bujumbura kabla ya mechi ya marudiano kuandaliwa jijini Nairobi majuma mawili baadaye. Mkufunzi mkuu Hassan Oktay angali likizoni baada ya kupata idhini ya kushughulikia masuala muhimu ya kifamilia.

Wiki jana, Gor Mahia walipangua mchuano wa kirafiki uliokuwa uwakutanishe na Al Hilal ya Sudan jijini Nairobi mnamo Alhamisi iliyopita. Mechi hiyo ilipaniwa kutoa jukwaa kwa mabingwa hao mara 18 na washikilizi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kujifua zaidi kwa kipute dhidi ya Noir.

Kujipiga msasa

Al Hilal kwa upande wao, walilenga kutumia mechi hiyo kujipiga msasa kadri wanavyojizatiti kupepetana na Rayon Sports ya Rwanda katika raundi ya kwanza ya mchujo wa mikondo miwili ya CAF.

Gor Mahia waliondolewa mapema kwenye CAF Champions League msimu jana na hivyo kushuka kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho (CAF Confederations Cup) ambapo walibanduliwa na Zamalek SC ya Misri kwenye hatua ya robo-fainali.

Wanapojiandaa kupiga hatua kubwa zaidi msimu ujao, watalazimika kuyakosa maarifa ya Shakava, Kahata na Tuyisenge walioyoyomea Zambia, Tanzania na Angola mtawalia.

Kwenye kampeni za kuwania ubingwa wa taji la CAF katika msimu wa 2017, Gor Mahia walibanduliwa katika raundi ya kwanza na Esperance ya Tunisia, tukio ambalo liliwashuhudia wakishuka ngazi kuwania Kombe la Mashirikisho barani Afrika ambapo walipangwa katika zizi moja na Yanga (Tanzania), USM Alger (Algeria) na Rayon Sports kutoka Rwanda.Hata hivyo, walishindwa kusonga mbele baada ya kilele cha kundi lao la D kutawaliwa na USM Alger na Rayon.