Michezo

Oliech ataambia watu nini?

February 24th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MIEZI miwili tu baada ya Dennis ‘The Menace’ Oliech kujiunga na Gor Mahia, mashabiki wanataka mabingwa hawa wa Kenya wamuadhibu mshambuliaji huyu kwa kumpiga kalamu baada ya kuigomea ikiwa na mechi muhimu ya Kombe la Mashirikisho la Afrika dhidi ya Hussein Dey ya Algeria mnamo Februari 24, 2019.

Ripoti zinasema Oliech hakufika katika kambi ya mazoezi Februari 22 na Februari 23 akilalamikia kulipwa sehemu ya mshahara wake wa mwezi Januari uliobaki na pia ada ya kununuliwa kwake.

Sehemu chache ya mashabiki imemtetea ikisema Gor bado inahitaji mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 34, lakini wengi wanaonekana walikerwa na tabia yake ya kugoma.

Shabiki KaGuya WuoMaggy anasema, “Oliech, kama ulisusia mechi hii, heri uende uendeshe hoteli ya Mama Oliech.”

Ujumbe huu ulipokelewa kwa hasira na mashabiki Muga Angaga na Ahmed Akida Wangara ambao walimtaka akome kutaja jina la mwendazake Mama Oliech, huku Anganga akiongeza kwamba Gor ilimkosa Oliech dhidi ya Dey.

Hata hivyo, KaGuya WuoMaggy amepata uungwaji mkono kutoka kwa Asienwa Bonnie, Austine Omollo, Jorge Mario Bergoglio, Oware Jefferson Wuoyi Siro na Tony Obiero.

“Kongole K’Ogalo, hiyo ni kazi safi. Kwa viongozi wa klabu ya Gor Mahia, wacheni Oliech aende; tunalipa fedha nyingi kwa mchezji huyu mmoja,” Asienwa Bonnie. Jorge Mario Bergoglio anasema, “Kile Oliech anaweza kufanya, Kahata na … wanaweza kufanya vizuri zaidi.”

Naye Oware Jefferson Wuoyi Siro anasema, “Gor Mahia, K’Ogalo Sirkal si ya mchezaji mmoja Oliech, lakini umakinifu na kuleta matokeo….Leo wameona, wamesikia tena wanashangaa.”

Tony Obiero, “Hongera Mighty Gor na Pole Sana kwa Oliech na wafuasi wake.”

Oliech alijiunga na Gor mnamo Januari 2, 2018 kwa kandarasi ya miaka miwili inayomvunia mshahara wa Sh350, 000 kila mwezi. Anasemakana yeye ndiye mchezaji anayelipwa mshahara wa juu Gor Mahia. Oliech, ambaye alijiunga na Gor baada ya kustaafu soka kwa karibu miaka mitatu, amefungia waajiri wake wapya mabao mawili, bao moja lilikuwa dhidi ya Zamalek kutoka Misri katika ushindi wa Gor wa mabao 4-2 uwanjani Kasarani mnamo Februari 3.