Michezo

Oliech atetea bwanyenye wa Wazito

July 13th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Harambee Stars Dennis ‘The Menace’ Oliech amemtetea mmiliki wa Wazito FC Ricardo Badoer ambaye amelaumiwa kwa kuwatusi wachezaji na kukatiza kandarasi zao bila kufuata sheria za leba.

Badoer ambaye ni bilionea kutoka Uswidi aliwatimua wachezaji 12 akiwataja kama wazembe ambao hawakuwa na msukumo wa ndani kuletea timu hiyo matokeo mazuri uwanjani.

Pia alisema hatua yake ilichochewa na kutoweza kuhimili mzigo wa kuwalipa mishahara baada ya biashara zake kuathirika vibaya kutokana na janga la virusi vya corona.

Baadhi ya wachezaji waliotimuliwa ni Victor Ndinya, Teddy Osok, Derrick Otanga, Lloyd Wahome, goalkeeper Steve Njung’e and Kevin Omondi. Wale wa kigeni walioangukiwa na shoka hilo ni Augustine Otu, Piscas Kirenge, Issioffu Bourahana, Paul Acquah.

Mshambuliaji tajika Paul ‘Modo’ Kiongera naye ameagana na klabu hiyo baada ya majadiliano ya kumwongezea kandarasi nyingine baada ya awali kukamilika mwezi uliopita, kusambaratika.

Hata hivyo, Oliech alieleza Taifa Leo kwamba Badoer hakufaa kutumia lugha ya matusi ila akaunga hatua yake ya kuwatimua kwa uzembe na ukosefu wa uwajibikaji.

“Mimi ninapenda watu ambao hudhibiti timu zao na hawavumili ukosefu wa uwajibikaji uwanjani. Utahisi vipi kama unawalipa wachezaji mishahara kila mwezi na matokeo ni mabaya uwanjani?” akauliza Oliech.

“Wachezaji wa timu kama Gor Mahia wamekosa mishahara kwa miezi kadhaa ilhali wenzao wa Wazito wamekuwa wakipokea hela kwa wakati lakini matokeo hakuna uwanjani. Badoer amekuwa akiwafuatilia na ilikuwa muda tu kabla ya shoka kuwaangukia,” akaongeza

Oliech ambaye pia alisakatia Gor Mahia na Mathare United enzi zake aliwarai wachezaji wa timu zinazomilikiwa na watu binafsi kujikaza kila mara wanapopata nafasi ya kucheza ili kuzuia kuchemkiwa hadharani jinsi alivyofanya Badoer.

“Hakuna mtu ambaye huwekeza kwa wachezaji wazembee hata kama ni tajiri kiasi gani. Kama Badoer angekuwa Mkenya, ningemrai awanie Urais wa FKF kwa sababu ni meneja anayefuatilia matukio kwa makini na kuwatuza wanaofanya bidii,” akasema.

Kando na kutimuliwa kwa wachezaji wa Wazito, aliyekuwa kocha Stewart Hall pia aliondoka baada ya kuafikiana na uongozi wa timu hiyo.

Duru zinaarifu kwamba Naibu kocha Fred Ambani huenda akapandishwa cheo na kuwa kocha wa Wazito kwa kuwa anaelewa timu hiyo na ni rafiki mkubwa wa Badoer.

Wazito wanashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 20 baada ya raundi 23 za mechi msimu huu.