Oliech kuandaa mechi kubwa ya kuwapa mashabiki fursa ya kumuaga rasmi kwenye ulingo wa usogora

Oliech kuandaa mechi kubwa ya kuwapa mashabiki fursa ya kumuaga rasmi kwenye ulingo wa usogora

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA wa zamani wa Harambee Stars, Dennis ‘The Menace’ Oliech, amefichua mipango ya kuandaa mechi ya kumuaga rasmi kwenye ulingo wa usogora mnamo Juni 2021.

Oliech aliduwaza wengi alipoangika daluga zake ghafla mnamo Januari 2019 katika hatua iliyotamatisha rasmi kipindi cha takriban miongo miwili ya kutamba kwake katika majukwaa ya kabumbu.

Kipindi kifupi baada ya Oliech kutangaza kustaafu kwake, mashabiki wa soka walisalia kusubiri kuchezwa kwa mechi ya kumuaga, jambo ambalo mshambuliaji huyo wa zamani wa AJ Auxerre ameahidi kufanikisha mwaka huu.

Oliech ambaye pia amewahi kusakatia FC Nantes ya Ufaransa, alifungia Harambee Stars jumla ya mabao 34, rekodi ambayo haijawahi kukaribiwa na fowadi yeyote mwingine wa timu hiyo ya taifa.

Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo, kutoandaliwa kwa mchuano wa kirafiki wa kumuaga rasmi kulichangiwa na uchechefu wa fedha pamoja na ujio wa janga la corona miezi miwili baada ya tangazo la kuangika kwake daluga kutolewa.

Nahodha huyo wa zamani wa Stars amefichua kwamba kwa sasa anajitahidi kushawishi wahisani na wafadhili mbalimbali kudhamini mchuano huo wa kumuaga ambao utajumuisha pia idadi kubwa ya wanasoka wa ughaibuni, raia wa humu nchini wanaopiga soka ya kulipwa katika mataifa ya kigeni na wachezaji wa soka ya humu nchini.

Nahodha wa sasa wa Harambee Stars Victor Wanyama, Mconald Mariga ambaye ni kakaye Wanyama pamoja na kiungo mtia-ladha, Jamal Mohammed ni miongoni mwa wachezaji ambao Oliech amefichua kwamba watanogesha mechi hiyo atakayoiandaa.

Oliech ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Gor Mahia, vilevile amefichua maazimio yake ya kuwania kiti cha urais wa Shirikisho la Soka la Kenya katika siku za usoni.

Kulingana naye, ipo idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, hasa katika bara la Ulaya, ambao wamekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara naye ili nia ya kufanikisha maandalizi ya mchuano huo wa kumpa ‘kwaheri’.

“Nimekuwa nikiwazia kuhusu uwezekano wa kuandaliwa kwa mechi ya kuniaga rasmi katika ulingo wa usogora. Sasa natarajia kwamba mchuano huo utapigwa mwaka huu. Ni mechi ambayo ikifanyika, itanipa fursa muhimu ya kuwaaga mashabiki wangu na kuwashukuru kwa jinsi ambavyo wameniunga mkono kwa miaka hii yote,” akatanguliza.

“Ilikuwa mipango yangu kuandaa mechi hiyo pindi baada ya kustaafu kwangu ila corona ikabisha na kupatikana kwa fedha za maandalizi kukawa vigumu. Maandalizi ya mechi ya kiwango hicho ni ghali,” akasema nyota huyo wa aliyewahi kuchezea kikosi cha Al-Arabi nchini Qatar kati ya 2003 na 2005.

“Nina orodha ndefu ya wanasoka wa ughaibuni ambao yatakuwa matamanio yangu wakinogesha kivumbi hicho kitakachosakatwa nje ya kalenda ya kawaida ya ligi mbalimbali. Nina imani kwamba kufikia mwisho wa kipindi cha maandalizi, ambacho natazamia kiwe cha miezi mitano, Covid-19 itakuwa imedhibitiwa vilivyo na hivyo kuwapa mashabiki idhini ya kuhudhuria mechi hiyo kwa wingi,” akaongeza.

Oliech ameongeza kwamba mechi hiyo itawaleta pamoja wanasoka wote waliowahi kuchezea timu ya taifa ya Harambee Stars katika miaka ya 80 na 90 ambao watahudhuria na hivyo kupata jukwaa la kuwaaga rasmi mashabiki wao waaminifu.

Kulingana naye, usimamizi wake utatumia mtandao wa kijamii kuwaomba Wakenya wateue wanasoka ambao wao wenyewe wangependa kushuhudia ama wakishiriki au kuhudhuria mchuano huo.

“Hakuna mwanasoka wa zamani wa Harambee Stars ambaye amewahi kupata jukwaa zuri na maridhawa zaidi la kuwaaga mashabiki wake. Nalenga kuwaalika wengi wao ili watoe shukran zao kwa mashabiki na ikiwezekana nao watambuliwe,” akaongeza Oliech ambaye pia amewahi kuchezea Dubai CSC.

Oliech aliwahi kujumuishwa na gazeti la The Guardian nchini Uingereza katika orodha ya wanasoka matata zaidi wanaowindwa duniani kutokana na utajiri wa vipaji vyao. Kwa wakati huo, orodha hiyo ilijumuisha pia Wayne Rooney na Robin van Persie walioishia kutamba vilivyo katika enzi zao za usogora.

Oliech aliwahi kupokezwa ofa ya mamilioni ya pesa ili abadilishe uraia wake na kuupata ule wa Qatar. Mbali na kuchezea Nantes, Auxerre na Ajaccio za Ufarasa, Oliech aliwahi pia kuchezea Dubai CSC katika Falme za Milki za Kiarabu almaarufu United Arab Emirates (UAE) kabla ya kuangika daluga zake akivalia jezi za Gor Mahia mnamo 2019.

You can share this post!

SPANISH CUP: Barcelona wapewa limbukeni Cornella...

Wakenya kujaribu bahati yao kwa mara nyingine katika Mbio...