Oliech kuwa mgeni wa heshima Bukhungu tuzo za SOYA

Oliech kuwa mgeni wa heshima Bukhungu tuzo za SOYA

Na GEOFFREY ANENE

MBIVU na mbichi kuhusu nani alifanya vyema kustahili kutuzwa mwanamichezo bora nchini Kenya mwaka 2021 itajulikana ugani Bukhungu katika kaunti ya Kakamega mnamo Januari 25.

Mshambuliaji wa zamani wa Harambee Stars Dennis Oliech atakuwa mgeni wa heshima kwenye tuzo hiyo maarufu kama SOYA ambayo ilianzishwa 2004 na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42, Paul Tergat.

Dereva wa kike Maxine Wahome (mbio za magari), mabingwa wa Olimpiki Faith Kipyegon (mbio za mita 1500) na Peres Jepchirchir (marathon) na Jentrix Shikangwa (soka) wanawania kuwa mwanamichezo bora mwanamke.

Mabingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge (marathon) na Emmanuel Korir (mita 800), mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala, mwanaraga wa Kenya Shujaa Alvin ‘Buffa’ Otieno na bingwa wa Afrika mbio za magari Carl Tundo ni wawaniaji wa mwanamichezo bora mwanamume.

Mshambuliaji Michael Olunga na mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 21 Peres Jepchirchir walishinda vitengo hivyo katika hafla ya kutuza waliong’ara 2020.

Washindi wa makala yaliyopita ya tuzo hiyo hawakuzawadiwa fedha. Hiyo ilikuwa kutokana na ukosefu wa wadhamini baada ya janga la virusi vya corona kufanya wasijitokeze. Tuzo za 2021 zimepokea jumla ya udhamini wa Sh4 milioni kutoka kwa kampuni ya Lotto, Safaricom na Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF). Kwa mujibu wa Rais wa chama cha waandishi habari za michezo Kenya (SJAK) Chris Mbaisi, anayehudumu katika jopo la kuchambua wanamichezo bora la SOYA, anasema tuzo ya kifedha itapeanwa Bukhungu japo ndogo. “Hali mbaya ya kiuchumi kutokana na janga la virusi vya corona haikuruhusu wadhamini kujitokeza 2021 kwa hivyo washindi hawakupokea fedha,” alieleza Mbaisi, Jumatatu.

Wanamichezo pamoja na maafisa kutoka mashirikisho mbalimbali ya michezo na serikali walimiminika mjini Kakamega hapo Jumatatu. Gavana wa Kaunti ya Kakamega, Wycliffe Oparanya pia atahudhuria hafla hiyo ya kifahari itakayoanza Jumanne saa kumi na mbili jioni. Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) Tergat na maafisa wengine kutoka kamati hiyo pia watakuwa Bukhungu.

Baadhi ya wawaniaji wengine wa 2021 ni wanaraga wa KCB (Timu ya bora ya mwaka – wanaume), mwanatenisi Selline Ahoya (Chipukizi aliyeinuka – msichana); mwanariadha Heriston Wanyonyi (Chipukizi aliyeinuka – mvulana); mwanavoliboli Sharon Chepchumba (Mwanamichezo wa mwaka – mwanamke); mwanariadha Wilson Bii (Mwanamichezo wa mwaka mwanamume (mlemavu); mnyanyuaji uzani Hellen Wawira (Mwanamichezo wa mwaka mwanamke – mlemavu).

Madhumuni ya tuzo hizi kutuza wanamichezo waliofanya vyema katika mwaka uliotangulia.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens kileleni licha ya sare

Oparanya kutetea kiwanda cha sukari

T L