Michezo

Olimpiki: Cherotich na Chepkoech ndani fainali ya 3,000m kuruka viunzi na maji

Na GEOFFREY ANENE August 4th, 2024 1 min read

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech pamoja na bingwa wa dunia chipukizi wasiozidi miaka 20 katika fani hiyo, Faith Cherotich, wamefuzu fainali huku Jackiline Chepkoech akiishiwa pumzi Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.

Wanadada hao wa Kenya walijikatia tiketi ya fainali baada ya kukamata nambari moja na mbili kwenye michujo yao Jumapili.

Cherotich, 20, ambaye alishinda nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia 2023 jijini Budapest, Hungary, alifuzu baada ya kukamilisha mchujo wa kundi la kwanza katika nafasi ya pili. Alikimbia vyema kutoka mwanzo hadi mwisho, ingawa alihitaji kufyatuka katika mita 70 za mwisho.

Mganda Peruth Chemutai alitawala kundi hilo kwa dakika 9:10.51 akifuatiwa na Cherotich (9:10.57), Mjerumani Felicitas Krause (9:10.68), Mwamerika Courtney Wayment (9.10.72) na Muethiopia Lomi Muleta (9:10.73).

Faith Cherotich (kulia) na Lomi Muleta wa Ethiopia wakishiriki mchujo wa kundi la kwanza. PICHA | REUTERS

Naye Chepkoech pia alifuzu fainali kwa kushinda kundi la tatu na mwisho katika dakika 9:13.56 pamoja na Mfaransa Alice Finot (9:14.78), Mjerumani Lea Meyer (9:14.85), Alicja Konieczek kutoka Poland (9:16.51) na Mhispania Irene Sanchez-Escribano (9:17.39).

Bingwa huyo wa dunia mwaka 2019 alimaliza Olimpiki za 2016 jijini Rio de Janeiro, Brazil, katika nafasi ya nne kisha nambari saba kwenye makala ya 2021 jijini Tokyo, Japan; hivyo, bado anatafuta medali yake ya kwanza ya Olimpiki.

Hata hivyo, Mkenya mwingine Chepkoech alibanduliwa katika kundi la pili baada ya kuvuta mkia. Bingwa wa dunia Winfred Yavi kutoka Bahrain, ambaye ni mzawa wa Kenya, pamoja na Muethiopia Sembo Almayew na Mwamerika Valerie Constien walinyakua nafasi tatu za kwanza kwa dakika 9:15.11, 9:15.42 na 9:16.33 katika kundi hilo mtawalia.

Watimkaji watano wa kwanza baada ya michujo ya Jumapili – washindi wa kila kundi na watimkaji wawili wengine waliokuwa na muda bora zaidi – watanogesha fainali Jumanne usiku.