Michezo

Olimpiki: Mabondia Wakenya waendelea kuzidiwa kwa makonde mazito mchujoni

February 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HUMPHREY Ochieng’ na Elizabeth Andiego wameingia katika orodha ndefu ya mabondia kutoka Kenya ambao ndoto yao ya kuwa katika Olimpiki 2020 nchini Japan imezimwa katika mchujo wa Bara Afrika unaoendelea mjini Dakar, Senegal.

Ochieng’ amelimwa na Mohamed Assaghir kutoka Morocco katika uzani wa kati ya kilo 75 na 81 (Light Heavy).

Elizabeth Andiego, ambaye alikuwa katika Olimpiki 2012 nchini Uingereza, amepoteza dhidi ya Randy Gramane kutoka Msumbiji katika robo-fainali ya uzani wa kati ya kilo 69-75 (uzani wa kati).

Shaffi Bakari katika uzani wa kati ya kilo ya 48 na 52 (Fly) na Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri katika uzani wa kati ya kilo 69 na 75 (uzani wa kati) waliaga mashindano katika raundi ya pili mnamo Februari 23.

Bakari alilemewa na Mghana Selemanu Tetteh kwa wingi wa alama naye Okwiri, ambaye hucheza ndondi za malipo, pia alizidiwa kwa wingi wa alama dhidi ya Mganda David Ssemujji.

Nahodha wa timu ya Kenya inayofahamika kwa jina la utani ‘Hit Squad’, Nick Okoth alimzaba Wilson Semedo (Cape Verde) kwa wingi wa alama na kuingia raundi ya 16-bora.

Hata hivyo, Okoth atakuwa na kibarua kigumu baadaye Jumatatu atakapolimana na Mmisri Mohamed Fahmi katika pigano lake lijalo katika kitengo cha uzani wa kati ya kilo 52 na 57 (Featherweight).

Christine Ongare pia alikuwa na mwanzo mzuri alimpomshinda Ornella Havyarimana kutoka Burundi katika uzani wa kati ya kilo 48 na 51 (Fly). Atachapana na Mondestine Munga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika pambano la robo-fainali.