Michezo

Olimpiki: Macho yote kwa Moraa fainali ya 800m

Na GEOFFREY ANENE August 5th, 2024 1 min read

BINGWA wa dunia mbio za mita 800, Mary Moraa, atatimka fainali ya Olimpiki leo usiku baada ya kutawala nusu-fainali yake kwa dakika 1:57.86 jijini Paris, Ufaransa.

Moraa – ambaye alibanduliwa katika nusu-fainali ya makala ya 2020 jijini Tokyo, Japan – alisubiri hadi kona ya mwisho kuonyesha wapinzani wenzake kisogo kwenye mbio hizo za kuzunguka uwanja mara mbili, hapo Jumapili, Agosti 4, 2024.

Bingwa huyo wa Jumuiya ya Madola 2022 kutoka Idara ya Polisi alifuzu moja kwa moja na Muethiopia Worknesh Mesele (1:58.06).

Muda bora wa Moraa, 24, mwaka huu ni dakika 1:56.71 aliopata katika riadha za Diamond League duru ya Eugene nchini Amerika mwezi Mei.

Moraa ndiye amebeba matumaini yote ya Kenya kupata medali katika mbio hizo kwani dakika chache baadaye Vivian Kiprotich hakuwa na lake katika nusu-fainali ya pili.

Kiprotich alikuwa mkiani kutoka mwanzo hadi mwisho akitamatisha kwa 1:59.64, huku Muethiopia Tsige Duguma (1:57.47) na Shafiqua Maloney kutoka St Vincent & Grenadines (1:57.59) wakijikatia tiketi kushiriki fainali kutoka kundi hilo.

Nusu-fainali ya tatu na mwisho ilishuhudia bingwa wa Kenya, Lilian Odira – ambaye alikamata nafasi ya pili kwenye Riadha za Afrika 2024 nchini Cameroon – akimaliza katika nafasi ya nne kwa 1:58.53.

Muingereza Keely Hodgkinson, ambaye amekuwa katika fomu bomba msimu huu na anajivunia kuwa nambari moja kwa muda bora mwaka huu, alizoa tiketi ya fainali kwa kushinda kundi hilo kwa 1:56.86 akifuatiwa na Prudence Sekgodiso (1:57.57).

Fainali ni leo Jumatatu usiku saa tano kasoro dakika 13.