Michezo

Olimpiki: Wanamichezo wapigania marupurupu mazuri, si vipeni vichache

May 31st, 2024 3 min read

NA WACHIRA MWANGI

KAMATI ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) inataka marekebisho yafanywe kwa sera ya marupurupu ya wanariadha, huku tarehe ya kuanza kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ikikaribia.

Rais wa NOC-K, Paul Tergat, alipokuwa akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Michezo, alisema kuwa wako katika mstari wa mbele kuhakikisha vipengele vyote vya maandalizi vinashughulikiwa kwa umakini.

Naye Mwekahazina wa NOC-K, Anthony Kariuki, alitaka suala la marupurupu ya wanariadha wakiwajibika ama wakiwa nchini au wakiwa nje, linafaa lipewe kipaumbele cha haraka.

Alisema hakujakuwepo na mabadiliko yoyote tangu mwaka 2018.

“Mapendekezo kuhusu marekebisho hayo yamewasilishwa kwa mamlaka husika, ambapo la muhimu ni malipo bora yanayozingatia gharama ya maisha ya sasa, viwango vya ubadilishanaji wa shilingi kwa dola ya Kimarekani miongoni mwa mengine, lakini bado hayajatekelezwa,” akasema Bw Kariuki akiiambia kamati hiyo.

Ili kurahisisha juhudi hizo, Bw Kariuki aliongeza kuwa makubaliano yameandaliwa, yakibainisha majukumu ya pande mbalimbali.

“Kimsingi, matayarisho ya michezo ya Olimpiki huandaliwa mapema sana lakini idhini na bajeti hutolewa mwezi mmoja kabla ya Olimpiki. Tuna bajeti na tunaukuma ili ipate idhini,” alieleza Bw Kariuki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo na Utamaduni, Daniel Wamalwa, alionyesha wasiwasi kuhusu ustawi wa wanamichezo, akibainisha kuwa Serikali ya Kenya kwanza inalenga kutuza vipaji kwa pesa kupitia Talanta Hela.

“Mnafanya nini kuhakikisha wanariadha ambao hawawezi kusafiri nje ya Kenya, wanaonyesha uwezo wao? Mnafanya nini kuhusu ustawi wa wanamichezo? Mnawalipa kiasi gani?” aliuliza Bw Wamalwa.

Katibu Mkuu wa NOC-K, Francis Mutuku, alisema kuwa Wizara ya Michezo huwa na wajibu muhimu kufanikisha ushiriki mzuri wa wanariadha wa Kenya katika michezo ya Olimpiki, ikiwemo ya Paris itakayofanyika kuanzia Julai 26, 2024 hadi Agosti 11, 2024.

Ikilinganishwa na miaka iliyopita, kamati ilibainisha kuwa wako tayari zaidi.

“Timu za kiufundi zimeundwa kuhakikisha nchi inapata ufanisi. Kwa mfano, katika riadha, hasa katika mbio za kupokezana vijiti, kamati imewasaidia wanariadha zaidi kuenda Afrika Kusini kwa mazoezi. Kwa upande mwingine, timu ya mpira wa kikapu au basketiboli ya wanawake haikufuzu, lakini msingi thabiti umewekwa kwa timu za baadaye,” alisema Bw Mutuku.

Juhudi zimeenea kimataifa, ambapo wanariadha wanasafiri kwenda Miramas, Ufaransa, kwa ajili ya kuzoea mazingira na kupata nafasi ya kufanya mazoezi na timu za huko.

Bw Mutuku alibainisha kuwa katika miaka miwili iliyopita, timu za taekwondo, mpira wa kikapu, na raga pia zimefaidika na kambi za mazoezi za kimataifa zilizoandaliwa na Timu ya Kenya almaarufu Team Kenya.

“Msaada wa afya ya akili kwa wanariadha kupitia ushirikiano na Hospitali ya Chiromo ni miongoni mwa yale ambayo tunajivunia. Ushirikiano wa kibiashara unaanzishwa ili kuwatambulisha na kuwaunga mkono wanariadha, na hatua za kuwalinda dhidi ya unyanyasaji na udhalilishaji zipo,” alieleza Bw Mutuku.

Aliongeza kuwa timu maalum zina mipango ya mazoezi ambapo timu ya raga itafanyia mazoezi yake jijini Madrid, ile ya voliboli nchini Serbia, na wanariadha na wakimbiaji wa masafa narefu watafanyia mazoezi Miramas kwa maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Paris.

Waogeleaji watashindana kwa viwango vya hadhi ya kimataifa na wenye alama za juu ndio wataiwakilisha Kenya.

Ili kuepuka matatizo kama yaliyotokea wakati wa Olimpiki za Rio nchini Brazil, ushirikiano na Kenya Airways umehakikisha usafari laini kwenda na kutoka Paris kwa wanariadha wote.

Makazi yatakuwa katika Kijiji cha Olimpiki, na wadhamini mbalimbali kama Safaricom, Kenya Breweries, na Multichoice watawapiga jeki washiriki.

Deloitte East Africa pia inashiriki katika kuboresha usimamizi na uwajibikaji.

Rais wa NOC-K Bw Tergat na mwekahazina Bw Kariuki, walibainisha umuhimu wa ushirikiano huu katika kuepuka kashfa na kuhakikisha wanariadha wanapata msaada mzuri.

Bw Kariuki alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa uwazi na uwajibikaji, ambao ulikuwa unakosekana wakati wa Olimpiki za Rio 2016.

Kama sehemu ya maandalizi, Kamati ilijulishwa kuwa wanariadha wamepata mafunzo ya kuwekeza katika fedha, namna ya kuzungumza na vyombo vya habari, na utambulisho wa kibinafsi.

Mafunzo ya ustadi wa maisha pia yanaangaziwa ili kuwasaidia wanariadha kuweza kuendesha maisha yao baada ya mashindano.

Mwakilishi kutoka Shirikisho la Riadha Nchini (AK) Dimmy Willy Kisalu, anayemwakilisha Rais wa AK Jackson Tuwei, alitoa wito kwa uongozi wa Kamati kufungua Uwanja wa Nyayo kwa ajili ya mashindano ya kufuzu kwa Olimpiki, akisema hiyo itatoa fursa kwa wanariadha wote wanaotaka kushiriki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo, Daniel Wamalwa, alitoa hakikisho kuwa mapendekezo yatazingatiwa ili kuhakikisha washiriki kutoka Kenya wanatia fora Paris.