Michezo

#Olimpiki2020: Wakenya 87 wafuzu

March 3rd, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA 87 wamefuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki 2020 itakayoandaliwa mjini Tokyo nchini Japan mnamo Julai 24 hadi Agosti 9.

Akizungumza katika hafla ya kutoa habari kuhusu masuala ya tiketi ya michezo hiyo katika afisi za Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOC-K), Kiongozi wa msafara wa timu ya Kenya, Waithaka Kioni aliongeza kuwa Kenya inatarajia kuwa na angaa wawakilishi 100 katika michezo hiyo ya kifahari kwa sababu bado mashirikisho mbalimbali yanaandaa mashindano ya kufuzu.

“Idadi hiyo ya wawakilishi wa Kenya ni nzuri, ingawa bado tunatarajia Wakenya zaidi kufuzu. Inajumuisha voliboli ya wanawake, raga ya wachezaji saba kila upanda ya wanaume na ile ya wanawake, taekwondo, masumbwi, uogeleaji na riadha,” alisema Mwenyekiti huyo wa Voliboli Kenya, ambaye pia ni naibu rais wa NOC-K na kutangaza kuwa kamati hiyo itatoa taarifa kuhusu hofu ya homa ya Coronavirus juma lijalo.

Kuhusu tiketi ni kuwa Wakenya watapata fursa ya mwisho kujinunuliwa tiketi za mashindano hayo Machi 16.

“Idadi ya watu wanaotaka tiketi ni kubwa hata kuliko ile ya Olimpiki 2016. Kuna ushindani mkali sana wa tiketi kwa hivyo Wakenya wanaombwa kujinyakulia tiketi hizo zitakapouzwa Machi 16 saa tatu asubuhi kwenye tovuti ya www.kingdomsg.com.

“Tiketi hazitauzwa tena baada ya kipindi hicho,” alisema Daniel Beniston, Mkurugenzi wa Kingdom Sports Group na kusisitiza kuwa ni kampuni hiyo pekee ilioruhusiwa kuuza tiketi.

“Mashindano haya ni makubwa na kama kawaida huwa hayakosi matapeli wa kuuza tiketi. Tunatahadharisha mashabiki kuwa Kingdom Sports Group ndio kampuni ilio na leseni ya kuuza tiketi za Olimpiki 2020.

“Hakuna haja ununue tiketi kutoka kwingineko kwa sababu hata ukifika Japan hutaruhusiwa kufika katika eneo la mashindano,” alionya afisa huyo ambaye alikuwa akizungumza baada ya kuongoza warsha kuhusu tiketi za michezo hiyo iliyokamilika jijini Nairobi.

Baadhi ya wanamichezo watakaopeperusha bendera ya Kenya kwenye Olimpiki 2020 ni washikilizi wa rekodi za mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge (wanaume) na Bridgid Kosgei (wanawake), Faith Ogalo (taekwondo) na Nick Okoth na Christine Ongare (masumbwi) ambao ni Wakenya wa hivi punde kufuzu.

Wachezaji wa voliboli ya ufukweni Brackcides Agala, Gaudencia Makokha, Phoscah Kasisi na Yvonne Wavinya watakabiliana na washiriki kutoka Cape Verde, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na wenyeji Nigeria katika raundi ya pili ya mchujo wa Afrika itakayoanza mjini Abuja, leo.

Mwaka 2016, Kenya iliwakilishwa na wanamichezo 89 katika Olimpiki mjini Rio de Janeiro nchini Brazil na kuzoa medali sita za dhahabu, sita za fedha pamoja na shaba moja.

Nishani hizo zote zilipatikana katika riadha, ingawa Kenya pia ilishiriki katika ulengaji shabaha, ndondi, judo, uogeleaji, unyanyuaji mizani na raga ya wachezaji saba kila upande.

Aidha, Kenya itapokonywa tiketi mbili ilizopatiwa kushiriki uogeleaji katika Olimpiki 2020 isipofanya uchaguzi wake hara iwezekanavyo.