Olivier Giroud pua na mdomo kusajiliwa na AC Milan

Olivier Giroud pua na mdomo kusajiliwa na AC Milan

Na MASHIRIKA

FOWADI mzoefu wa Chelsea, Olivier Giroud yuko pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya AC Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 anatarajiwa kutia saini mkataba wa miaka miwili na AC Milan wakati wowote kuanzia sasa.

Giroud alisajiliwa na Chelsea kwa kima cha Sh2.8 bilioni kutoka Arsenal mnamo Januari 2018. Alitia saini mkataba mpya wa kuhudumu uwanjani Stamford Bridge hadi 2022 mnamo Juni 2021.

Katika msimu wa 2020-21, Giroud alichezea Chelsea mara 31 na akapachika wavuni jumla ya mabao 11.

Baada ya Chelsea kuwasajili mafowadi Kai Havertz na Timo Werner, Giroud alijipata akisugua benchi mara kwa mara na akapangwa kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hao mara nane pekee mnamo 2020-21.

Kufikia sasa, Giroud amefungia Chelsea jumla ya mabao 39 kutokana na michuano 119 huku akisaidia waajiri wake hao kutia kapuni taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Europa League na Kombe la FA.

Giroud ambaye alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia Ufaransa ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, aliwahi kuongoza Arsenal kutawazwa mabingwa wa Kombe la FA mara tatu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Dkt Ruto afichua alichomnong’onezea Rais katika ukumbi wa...

Ogier arudisha mkono kwa kumwaga Sh2.4 milioni kusaidia...