Michezo

Olunga afungia Kashiwa Reysol bao la ushindi

August 19th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Mshambuliaji Michael Olunga alirejeshwa kikosini na kocha Nelsinho Baptista na ‘kurudisha mkono’ kwa kuwa na imani naye alipopachika bao la ushindi Kashiwa Reysol ikizamisha V-Varen Nagasaki 2-1 ligini Agosti 17, 2019.

Olunga hakuchezeshwa katikati mwa wiki Kashiwa ikibanduliwa nje ya kombe la muondoano la Emperor’s Cup kwa kuchapwa 1-0 na Sagan Tosu.

Hat hivyo, alidhihirisha umuhimu wake katika kampeni ya Kashiwa kurejea katika Ligi Kuu alipofuma wavuni bao la ushindi dhidi ya V-Varen dakika ya 75.

Mbrazil Matheus Savio aliweka Kashiwa kifua mbele dakika ya tisa, lakini V-Varen ikasawazisha kupitia penalti ya Hiroto Goya dakika ya 50.

Ushindi huu wa 10 mfululizo wa Kashiwa kwenye Ligi ya Daraja ya Pili unadumisha uongozi wake hadi alama 58. Kashiwa imefungua mwanya wa alama saba juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 22. Imenufaika pakubwa kuweka pengo hilo kubwa baada ya nambari mbili Kyoto kulimwa 3-0 na Mito, Jumamosi. Timu mbili za kwanza pekee baada ya kila timu kusakata mechi 42 ndizo zitapandishwa daraja.

Wachezaji 11 wa kwanza – Nakamura (Kipa), Koga, Someya, Kamata, Kawaguchi, Richardson, Mihara, Savio, Segawa, Esaka, Olunga. Wachezaji wa akiba – Kirihata (Kipa), Yamashita, Otani, Kobayashi, Tanaka, Santos, Unoki.

Olunga alikosa mechi ya Jumatano ambayo timu yake ya Kashiwa ilipoteza 1-0 dhidi ya Sagan Tosu kwenye soka ya Emperor’s Cup.

Kashiwa, ambayo ilinyakua kombe hili mwaka 1972, 1975 na 2012, iliingia mchuano wa Sagan Tosu na motisha ya kutoshindwa msimu huu katika mechi 11 ikiwemo kushinda 10 zilizopita.

Hata hivyo, ilimaliza mechi tatu mfululizo dhidi ya Sagan bila ushindi baada ya kuchapwa 1-0 katika muda wa ziada. Dakika 90 zilikamilika 0-0 kabla ya nyota wa zamani wa Uhispania, Fernando Torres, 35, kufungia Sagan bao hilo muhimu katika uwanja wa nyumbani wa Kashiwa wa Hitachi Kashiwa.

Kashiwa ilikamilisha mechi hii watu 10 baada ya mchezaji wake mmoja kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 116.

Sagan iko katika mduara hatari wa kutemwa kutoka Ligi Kuu ya Japan katika nafasi ya 16 nayo Kashiwa inaongoza Ligi ya Daraja ya Pili.

Kocha Baptista hakumchezesha mshambuliaji Olunga katika mchuano huu siku chache tu baada ya Mkenya huyo kuchana nyavu mara tatu Kashiwa ikibwaga Renofa Yamaguchi 4-1 kwenye ligi.