Michezo

Olunga amega pasi mbili zilizozalisha magoli

August 6th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Kashiwa Reysol anayochezea Mkenya Michael Olunga iliandikisha ushindi wake wa nane mfululizo na kuendelea kujiweka pazuri kurejea kwenye Ligi Kuu ya Japan baada ya kulipua Ryukyu 5-1 katika ligi ya daraja ya pili Jumapili.

Katika mchuano huo wa 26 kwenye ligi hiyo ya klabu 22, mshambuliaji Olunga alicheza dakika 83 na kumega pasi zilizozalisha mabao mawili kabla ya kiungo Mbrazil Matheus Savio kujaza nafasi yake.

Wageni Ryukyu walitangulia kuona lango kupitia kwa mshambuliaji Koji Suzuki dakika ya 31. Hata hivyo, Kashiwa ilifurahia uongozi wa mabao 2-1 wakati wa mapumziko baada ya kujibu na mabao kutoka kwa kiungo Yusuke Segawa na beki Taiyo Koga dakika ya 39 na 42 mtawalia.

Matumaini ya Ryukyu kurejea kwenye mechi yalizimwa kabisa pale Kashiwa ilipoongeza mabao kupitia kwa viungo Ataru Esaka na Mbrazil Cristiano katika dakika 15 za kwanza za kipindi cha pili kabla ya Esaka kugonga msumari wa mwisho dakika ya 90.

Kashiwa inasalia kileleni kwa alama 52. Iko alama mbili mbele ya Kyoto ambayo ilinyamazisha Verdy 4-0, nayo Omiya Ardija iko alama nne nyuma katika nafasi ya tatu baada ya kuchapa Motendio Yamagata 3-2.

Timu mbili zitakazokamilisha msimu katika nafasi mbili za kwanza zitapandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Kashiwa itavaana na Renofa Yamaguchi katika mechi yake ijayo Agosti 10. Klabu za Tochigi na Gifu zinashikilia nafasi mbili za mwisho katika Ligi ya Daraja ya Pili na katika hatari ya kutupwa ligi ya daraja ya tatu.