Michezo

Olunga aomba asiichezee Harambee Stars

May 21st, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA itakosa huduma mfungaji wake matata wa wakati huu, Michael Olunga katika mechi za kirafiki dhidi ya Swaziland (Mei 25) na Equatorial Guinea (Mei 28).

Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 24 ameomba ruhusa kuachwa nje ya michuano hii kutokana majukumu ya klabu yake ya Girona nchini Uhispania.

Olunga amefungia Stars mabao sita katika mechi nane zilizopita. Aliona lango Kenya ilipotoka 1-1 dhidi ya Uganda katika mechi ya kirafiki Machi 23, 2017 na mabao mawili katika mechi nyingine ya kujipima nguvu ambayo Stars ililemea DR Congo 2-1 Machi 26, 2017.

Pia alicheka na wavu mara moja dhidi ya Sierra Leone katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019, ambayo Stars ilipoteza 2-1 (Juni 10, 2017) na kupata bao moja katika mechi za kirafiki ambayo Iraq ilishinda 2-1 Oktoba 5, 2017.

Katika mechi ya mwisho Stars ilicheza, Olunga alisukuma wavuni bao moja, huku Kenya ikibwagwa 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) hapo Machi 27, 2018. Mchuano huu pia ulikuwa wa kirafiki.

Kocha Mkuu wa Stars, Sebastien Migne, hata hivyo, anatarajiwa kupata huduma za Olunga katika shindano la kimataifa la Hero Intercontinental Cup litakaloandaliwa nchini India kutoka Juni 1 hadi Juni 10 mjini Mumbai.

Stars itaingia kambini Mei 21 katika Chuo cha Mafunzo ya Kifedha (KSMS) mtaani Ruaraka kujiandaa kwa mechi dhidi ya Swaziland na Equatorial Guinea. Wachezaji wa kimataifa wanaotarajiwa kufika mazoezini kesho ni Ismael Gonzalez (CF Fuenlabrada, Uhispania), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, Uingereza), McDonald Mariga (Real Oviedo, Uhispania), Ayub Timbe (Heilongjiang, Uchina), Eric Ouma (KF Tirana) na Masoud Juma (Cape Town City, Afrika Kusini).

 

Kikosi cha Stars cha mechi dhidi ya Swaziland na Equatorial Guinea: 

Makipa – Patrick Matasi (Posta Rangers), Boniface Oluoch (Gor Mahia), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars);

Mabeki – Jockins Atudo (Posta Rangers), Musa Mohammed (hana klabu), Harun Shakava (Gor Mahia), Joash Onyango (Gor Mahia), Bolton Omwenga (Kariobangi Sharks), Michael Kibwage (AFC Leopards), Philemon Otieno (Gor Mahia), Eric Ouma (KF Tirana);

Viungo – Ismael Gonzalez (CF Fuenlabrada, Uhispania), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, Uingereza), McDonald Mariga (Real Oviedo, Uhispania), Ayub Timbe (Heilongjiang, Uchina), Humphrey Mieno (Gor Mahia), Francis Kahata (Gor Mahia), George Odhiambo (Gor Mahia), Duncan Otieno (AFC Leopards), Whyvonne Isuza (AFC Leopards);

Washambuliaji – Masoud Juma (Cape Town City, Afrika Kusini), Pistone Mutamba (Wazito FC), Ovella Ochieng (Kariobangi Sharks).

Wachezaji wa ziada: Michael Olunga (Girona FC, Uhispania), Marvin Omondi (AFC Leopards), Patillah Omotto (Kariobangi Sharks), Dennis Sikhayi (AFC Leopards), Johnstone Omurwa (Mathare United), Jafari Owiti (AFC Leopards), Robert Arot (Nakuru All Stars), Geoffrey Shiveka (Kariobangi Sharks), Chrispin Oduor (Mathare United)

Ratiba ya Harambee Stars (2018):

Mei 25 – Kenya vs. Swaziland (Kasarani)

Mei 28 – Kenya vs. Equatorial Guinea (Kasarani)

Juni 2 – Kenya vs. New Zealand (Hero Intercontinental Cup, India)

Juni 4 – India vs. Kenya (Hero Intercontinental Cup, India)

Juni 8 – Chinese Taipei vs. Kenya (Hero Intercontinental Cup, India)

Septemba 7 – Kenya vs. Ghana (mechi ya kufuzu AFCON 2019)

Oktoba 10 – Ethiopia vs. Kenya (mechi ya kufuzu AFCON 2019)

Oktoba 13 – Kenya vs. Ethiopia (mechi ya kufuzu AFCON 2019)

Novemba 16 – Kenya vs. Sierra Leone (mechi ya kufuzu AFCON 2019)