Michezo

Olunga atazama timu yake mpya ikinyanyaswa

August 13th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU mpya ya mvamizi Mkenya Michael Olunga, Kashiwa Reysol iliendelea kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu ya Japan (J1 League) baada ya kupapurwa mbele ya mashabiki wake 2-0 na Vegalta Sendai, Agosti 11, 2018.

Olunga, ambaye alitambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Reysol mnamo Agosti 10 baada ya kugura Ghizou Zhicheng nchini Uchina, alikuwa shabiki katika mchuano huu kwa sababu hakutumiwa.

Baada ya kipindi cha kwanza kukamilika bila bao, Reysol ilijipata chini 0-1 baada ya Hiroaki Okuno kufungia Sendai dakika ya 59. Matumaini ya Reysol kurejea kwenye mechi yalizimwa kabisa pale Sendai ilipopata bao la pili kupitia Takuma Nashimura dakika ya 80.

Kichapo hiki kinasukuma Reysol nafasi moja chini hadi nambari 13 kwa alama 23 kutokana na mechi 20 kwenye ligi hii ya klabu 18. Sendai nayo inaruka juu nafasi moja hadi nambari 12 kwa alama 26 kutokana na idadi sawa ya mechi.

Ni mechi ya nane mfululizo ambayo Reysol haijapata ushindi dhidi ya Sendai. Olunga, ambaye alisakata soka yake ya malipo katika Ligi Kuu ya Uhispania msimu uliopita katika klabu ya Girona kwa mkopo kutoka Zhicheng, huenda akacheza mechi yake ya kwanza Agosti 15 wakati Reysol itavaana na wenyeji FC Tokyo wanaoshikilia nafasi ya pili kwa alama 40.