Olunga ayoyomea Qatar ‘kumumunya mamilioni’

Olunga ayoyomea Qatar ‘kumumunya mamilioni’

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Michael Olunga alihiari kuyoyomea nchini Qatar usiku wa Januari 11, 2020 kuchezea kikosi cha Al Duhai SC baada ya kuvunja ndoa na klabu ya Kashiwa Reysol ya Ligi Kuu ya Japan (J1 League).

Hatua hiyo ya Olunga inamfanya kuwa Mkenya wa pili baada ya nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Dennis ‘The Menace’ Oliech kucheza soka ya kulipwa nchini Qatar. Taifa hilo liliwahi kumpokeza Oliech ofa ya mamilioni ya pesa (Sh200 milioni) ili abadilishe uraia wake na kupata ule wa Qatar.

Mbali na kuchezea Nantes, AJ Auxerre na AC Ajaccio za Ufarasa, Oliech aliwahi pia kuchezea Dubai CSC katika Falme za Kiarabu (UAE) kabla ya kuangika rasmi daluga zake akivalia jezi za Gor Mahia mnamo 2019.

 Chini ya kocha Sabri Lamouchi ambaye ni raia wa Ufaransa, Al Duhail waliotawazwa wafalme wa Ligi Kuu ya Qatar mnamo 2010-11, 2011-12, 2013-14, 2014-15, 2016-17, 2017-18 na 2019–20, kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali la vikosi 12. Kikosi hicho kinajivunia alama 27, nane nyuma ya viongozi Al Sadd SC wanaotiwa makali na kiungo mahiri wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Xavi Hernandez.

Kwa mujibu wa ripoti nchini Qatar na Japan, Olunga anatarajiwa sasa kutia mfukoni kima cha Sh14 milioni kwa wiki nchini Qatar, pesa hizo zikidi kwa mbali mshahara wa Sh8.3 milioni ambao nahodha wa Stars, Victor Wanyama alikuwa akipokezwa na Tottenham Hotspur ya Uingereza kabla ya kutua Canada kuchezea Montreal Impact mwanzoni mwa mwaka jana. Akiwa Reysol, Olunga alikuwa akipokea ujira wa takriban Sh8 milioni mwishoni kwa kila juma.

Kwa kujiunga na Al Duhail ambao ni mabingwa mara saba wa Ligi Kuu ya Qatar, Olunga anatarajiwa kuwa kizibo cha aliyekuwa mwanasoka nguli wa Bayern Munich, Mario Mandzukic, 34.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, iliripotiwa kwamba Reysol walikuwa wamekubali ofa ya Sh806 milioni kwa minajili ya kufanikisha uhamisho wa Olunga hadi Al-Duhail wanaomilikiwa na mfanyabiashara bwanyenye, Abdullah bin Nasser bin Al Ahmed Al Thani.

Mnamo Disemba 2020, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilimtia Olunga katika orodha ya wanasoka watano wa haiba kubwa ambao hawajulikani sana licha ya kuwika mno katika kampeni za mwaka wa 2020.

“Iwapo nitalazimika kuondoka Japan, basi itamaanisha kwamba ofa mpya nitakayokuwa nimepata ni ya kuridhisha zaidi kiasi kwamba itakuwa vigumu kabisa kuipuuza,” akasema fowadi huyo wakati huo.

Olunga alijivunia msimu wa kuridhisha katika kampeni za J1 League mnamo 2020 na akatawazwa Mchezaji Bora na Mfungaji Bora baada ya kucheka na nyavu za wapinzani mara 28 kutokana na mechi 32.

Katika mechi yake ya mwisho ndani ya jezi za Reysol, Olunga alifunga bao ila waajiri wake wakapokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa FC Tokyo kwenye fainali ya kuwania ubingwa wa taji la Levain Cup mnamo Januari 4, 2021.

Makali ya Olunga mbele ya malango ya wapinzani yalisaidia Reysol kukamilisha kampeni za msimu wa 2020 kwenye J1 katika nafasi ya saba jedwalini licha ya kwamba walipandishwa ngazi mwishoni mwa muhula uliotangulia ambao ulimshuhudia sogora huyo wa zamani wa Liberty Sports Academy, Tusker na Thika United akifunga magoli 27.

Ingawa Olunga amewahi pia kuchezea nchini Uswidi, Uhispania na China, wepesi wake wa kufunga mabao ulidhihirika zaidi katika kipindi cha misimu miwili iliyopita nchini Japan, ufanisi uliomfanya kuwa kivutio cha klabu kadhaa maarufu za bara Ulaya zikiwemo Olympique Lyon (Ufaransa), CSKA Moscow (Urusi) na Galatasaray (Uturuki).

“Mafanikio yangu kufikia sasa katika ulingo wa soka ni zao la imani na bidii. Sikuwahi kutamauka hata nilipojikuta nikikabiliwa na changamoto tele. Natambua pia ukubwa wa mchango wa wachezaji wenzangu katika vikosi vyote ambavyo nimewahi kuvisakatia,” akasema Olunga katika mahojiano yake ya awali na mtandao wa Fifa.com.

Kati ya rekodi nyinginezo zinazojivuniwa na Olunga katika ulingo wa soka ni kuwahi kuwa sogora wa kwanza kufungia FC Girona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) jumla ya mabao matatu katika mechi moja ligini.

Olunga aliwahi pia kufungia Reysol jumla ya mabao manane katika ushindi wa 13-1 uliosajiliwa na kikosi hicho dhidi ya Kyoto Sanga katika Ligi ya Daraja la Pili mnamo 2019.

Kabla ya kujiunga na Girona kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China ambayo ilimuuza kwa Sh56 milioni, Olunga aliwahi pia kusakata soka ya kulipwa kambini mwa Djurgardens IF ya Uswidi mnamo 2016.

Nyota huyo amekuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya Harambee Stars na mabao yake dhidi ya Ghana na Ethiopia yalisaidia Kenya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2019 nchini Misri.

Olunga alifungia Stars mabao matatu kwenye fainali hizo zilizoshuhudia Kenya ikibanduliwa mapema kwenye Kundi C lililojumuisha pia Tanzania, Senegal na Algeria waliotawazwa wafalme hatimaye baada ya kupiga Senegal 1-0 kwenye fainali.

You can share this post!

WALLAH BIN WALLAH: Usitumie nguvu za kifua unapofanya kazi,...

Ninapolewa na kuvuta bangi, ajuza wote hugeuka vipusa,...