Michezo

Olunga azamisha Gamba Osaka

February 17th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Mshambuliaji matata Michael Olunga alifuma wavuni bao la pekee timu yake ya Kashiwa Reysol ikizamisha wenyeji Gamba Osaka 1-0 katika kombe la muondoano la League Cup (YBC Levain Cup) uwanjani Suita nchini Japan, Jumapili.

Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye alifunga msimu uliopita kwa kutikisa nyavu za Kyto mara nane Kashiwa ikitamba 13-1 kwenye Ligi ya Daraja ya Pili na kurejea Ligi Kuu baada ya msimu mmoja chini, alipokea pasi safi kutoka kwa kiungo Yusuke Segawa ndani ya kisanduku na kukamilisha kupitia mguu wake wa kulia dakika ya 24.

Mabingwa wa Levain Cup mwaka 1999 na 2013 Kashiwa Reysol sasa watamenyana na Shonan katika raundi ya pili mnamo Februari 26. Shonan ilizima Oita 1-0 katika mechi nyingine ya raundi ya kwanza.

Kabla ya kukutana na Shonan, Kashiwa ya kocha Mbrazil Nelsinho Baptista itapepetana na Hokkaido Consadole Sapporo katika mechi yake ya ufunguzi ya Ligi Kuu mnamo Februari 22.

Matokeo (Februari 16, 2020): Cerezo Osaka 4-1 Yamaga, Gamba Osaka 0-1 Kashiwa Reysol, Shonan 1-0 Oita, Kawasaki Frontale 5-1 Shimizu, Nagoya 1-0 Kashima, Sagan Tosu 0-3 Sapporo, Urawa 5-2 Vegalta Sendai, Yokohama 0-2 Hiroshima.