Michezo

Olunga, Johanna na Wanyama wafurahisha waajiri wao katika soka ya majuu

August 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA wa Harambee Stars, Eric Johanna, Victor Wanyama na Michael Olunga walitambisha vikosi vyao katika soka ya inayopigwa na vikosi vyao vya ughaibuni.

Nchini Uswidi, Johanna aliwafungia Sodra bao moja katika ushindi wa 2-0 waliousajili dhidi ya Trelleborg. Ushindi huo uliwapaisha hadi nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Superettan.

Johanna alitikisa nyavu za wapinzani katika dakika ya tisa na kuwaweka waajiri wake uongozini kabla ya Trelleborg kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili. Johanna atakuwa sehemu ya kikosi cha Sodra kitakachovaana na AFC Eskilstuna katika kibarua kijacho ligini mnamo Septemba 2.

Nchini Japan, Olunga alifunga mabao mawili katika mchuano ulioshuhudia kikosi chake cha Kashiwa Reysol kikipokezwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa Misao.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilikamilika bila bao lolote.

Ilikuwa hadi dakika ya 57 ambapo Olunga aliwafungulia waajiri wake ukurasa wa mabao kabla ya Kshima Antlers kusawazisha mambo kunako dakika ya 72.

Olunga alipachika wavuni bao la pili katika dakika ya 84 kabla ya wageni wao kufunga magoli mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili.

Wanyama ambaye ni nahodha wa Harambee Stars aliwajibishwa kwa dakika 90 katika mechi iliyoshuhudia waajiri wake Montreal Impact wanaonolewa na kocha Thierry Henry wakilazwa 1-0 na Toronto FC kwenye Major League Soccer (MLS).

Ilikuwa pigo jingine kwa Mkenya Johanna Omollo baada ya chombo cha waajiri wake Cercle Brugge kuzamishwa na Kortrijk kwa bao 1-0 katika Ligi Kuu ya Ubelgiji.