Michezo

Olunga mawindoni kusaidia Kashiwa Reysol kumaliza rekodi duni ya mechi nne bila ushindi nyumbani

December 8th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI matata Michael Olunga atatumai kusaidia Kashiwa Reysol kumaliza ukame wa mechi nne bila ushindi mbele ya mashabiki wao wa nyumbani uwanjani Sankyo Frontier wakati klabu hiyo itaalika Oita Trinita kwenye Ligi Kuu ya Japan hapo Jumatano.

Vijana wa kocha Nelson Baptista watajibwaga uwanjani kwa mchuano huo baada ya kuandikisha ushindi mmoja kutoka mechi saba zilizopita uwanjani Sankyo Frontier. Hawana ushindi katika mechi nne mfululizo nyumbani.

Katika orodha ya mechi saba zilizopita, Kashiwa wamepokea vichapo kutoka kwa Yokohama F. Marinos 3-1, Sagan Tosu 2-1 na, juma lililopita, walilemewa 1-0 dhidi ya Nagoya Grampus. Kashiwa wamegawana alama na Shimizu S-Pulse (0-0) na majirani Urawa Red Diamonds (1-1). Ushindi wa pekee Kashiwa wamezoa mbele ya mashabiki wao katika mechi saba zilizopita ulikuwa 4-3 dhidi ya Vissel Kobe anayochezea gunge wa Uhispania Andreas Iniesta.

Dhidi ya nambari 11 Oita, nambari nane Kashiwa itakutana na timu inayoonekana dhaifu baada ya kuambulia alama moja katika mechi tatu zilizopita. Hata hivyo, Kashiwa itajilaumu ikidharau Oita ambayo imepoteza mechi moja ugenini kutoka orodha ya saba zilizopita.

Mchezaji wa kimataifa wa Kenya, Olunga, ambaye amehangaisha wapinzani J1 League msimu wote na urefu wake na kasi ya kutisha, atategemewa tena kutafuta kumaliza msururu huo wa mechi nne bila ushindi nyumbani.

Olunga, 26, amepachika mabao 26 kati ya 56 ambayo Kashiwa imepata kwenye ligi hiyo ya klabu 18 msimu huu. Alinyamazishwa na ulinzi mkali kutoka kwa Nagoya wikendi iliyopita katika mechi ambayo baadaye alikiri ilikuwa ngumu, lakini “waliyopata mafunzo kadhaa mazuri.”

Kashiwa italazimika kujituma kabisa ili kunyamazisha Oita ambayo kiungo wake nyota Naoki Nomura amenukuliwa na tovuti ya klabu hiyo akisema kuwa Oita “itapigana hadi kipenga cha mwisho”.

Mchuano huu uliratibiwa kusakatwa Novemba 14, lakini ukasukumwa hadi Desemba 9 baada ya kambi ya Kashiwa kupatikana na visa 16 vya maambukizi ya virusi hatari vya corona.

Utakuwa na mvuto wa aina yake kwa Olunga kwa sababu tiketi zake zimechapishwa na picha ya Olunga.

Mechi ya mkondo wa kwanza ilitamatika 0-0 mjini Oita mwezi Agosti. Kashiwa ina rekodi nzuri dhidi ya Oita. Haijashindwa katika mechi tatu zilizopita. Ilizaba Oita 2-0 mwaka 2017 kwenye Kombe la Emperor’s na kung’ara 3-1 kwenye Kombe la Levain mwezi Agosti.

Mara ya mwisho Oita ilivuna ushindi dhidi ya Kashiwa ilikuwa mwaka 2013 ilipotamba 1-0 kwenye Emperor’s Cup.

Engineer, jinsi Olunga anafahamika kwa jina la utani, amefungua mwanya wa magoli tisa juu ya jedwali la wafungaji. Mbrazil Everaldo ndiye mpinzani wake wa karibu. Amefungia Kashima Antlers mabao 17.

Inamaanisha kuwa Olunga ana nafasi kubwa ya kutawazwa mfungaji bora wa J1 League msimu huu wakati wa tuzo za ligi hiyo za mwaka 2020 zitakazofanyika Desemba 22. Tuzo hizo zitafanyika kupitia mtandao kutokana na janga la virusi vya corona.