Michezo

Omala: Nimeiva sasa kuvaa viatu vya Olunga huko Harambee Stars

Na CECIL ODONGO September 2nd, 2024 2 min read

MVAMIZI wa Harambee Stars Benson Omala amesema kuwa yupo tayari kujaza nafasi ya Michael Olunga kwenye mechi za kufuzu Kombe la Afrika 2025 (AFCON 2025).

Harambee Stars ipo katika kundi J na itatifuana na Zimbabwe mnamo Ijumaa.

Stars itakuwa mwenyeji wa mechi hiyo katika uga wa Mandela, Kampala, Uganda kwa sababu Kenya haina uga ambao umetimiza viwango vya CAF na FIFA ili kuandaa mechi za kimataifa.

Siku nne baadaye, Kenya itatembelea Namibia katika uga wa Orlando, Johannesburg Afrika Kusini.

Namibia pia haina uga ambao umefikia viwango vya Fifa na Caf kuandaa mechi za kimataifa.

Mabingwa mara tano wa Kombe la Afrika Cameroon pia wapo kwenye kundi hilo.

Timu mbili zitakazowika kwenye kila kundi katika makundi 12 zitatua nchini Morocco kushiriki Afcon makala ya 2025.

Licha ya Olunga kuandamwa na jeraha ambalo limemweka mkekani na kukosa kuchezea Al-Duhail ya Qatar mechi mbili zilizopita, Kocha Engin Firat alimjumuisha katika kikosi chake cha watu 25 watakaocheza dhidi ya Zimbabwe na Namibia.

Harambee Stars inatarajiwa kuelekea Uganda Jumatatu asubuhi.

Omala: Nimeiva sasa

Mnamo Jumapili, Omala, 22,  alisema kuwa sasa ameiva kusakatia Harambee Star na yupo tayari kuongoza safu ya mbele ya Stars.

“Kila mchezaji anastahili kuwa tayari wakati wowote. Nimekuwa katika kikosi na nimejifunza mengi kutoka kwa Olunga na iwapo nitapewa nafasi, nitajituma sana,” akasema Omala ambaye mwezi uliopita alijiunga na Al Safa inayoshiriki Ligi Kuu ya Lebanon.

Mabao 19

Omala alifunga mabao 19 msimu uliopita kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na kutwaa Kiatu cha Dhahabu pamoja na kuongoza Gor kutwaa ubingwa wa 21 wa ligi.

Firat alisema Olunga atajiunga na timu kule Uganda na ni uchunguzi wa kimatibabu (MRI) utaamua iwapo atakuwa fiti kucheza au la.

“Uwezekano wake wa kucheza ni finyu sana. Hatutakuwa na wachezaji wengi sana tegemeo na lazima tusake suluhu,” akasema Firat.

Kutokuwepo kwa Olunga ni pigo kwa Stars ikizingatiwa amekuwa tegemeo sana katika safu ya mbele.

Mnamo Machi alifunga mabao matano katika kipute cha Mataifa Manne (Four Nations Tournament)  kilichoandaliwa Lilongwe Malawi.

Kando na Omala, washambulizi wengine ambao Firat atawategemea ni Jonah Ayunga anayecheza soka ya kulipwa Scotland na John Avire.

Katika safu ya nyuma Firat pia atamkosa Collins Sichenje anayesakatia FK Vojvodina kule Serbia kutokana na jeraha.