Habari

Omanga amezea mate kiti cha naibu spika katika seneti

May 29th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA maalum anayekabiliwa na hatari ya kufurushwa kutoka chama cha Jubilee Millicent Omanga ni miongoni mwa maseneta sita ambao wanaumezea mate wadhifa wa Naibu Spika uliosalia wazi baada ya Kithure Kindiki kufurushwa.

Seneta huyo sasa anasubiri hatima yake baada ya kudadisiwa na Kamati ya Nidhamu ya chama hicho Jumatano kwa kususia mkutano wa maseneta wa Jubilee ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Mei 11, 2020.

Akijitetea mbele ya kikao cha Kamati hiyo katika makao makuu ya Jubilee, Nairobi, Bi Omanga alishikilia kuwa hakupokea ujumbe wa mwaliko kwa simu yake, ulidaiwa kutumwa na kiranja wa wengi Irungu Kangáta.

Hata hivyo, alikariri kwamba yeye ni mwaminifu kwa chama hicho tawala na uongozi wake na yu tayari kuunga mkono misimamo na maamuzi yake yote ndani n nje ya seneti.

Maseneta wengine ambao wamewasilisha maombi yake kwa wadhifa huo ni Margaret Kamar (Seneta wa Uasin Gishu, Jubilee), Charles Kabiru (Kiranyaga, Seneta wa Kujitegemea), Isaac Mwaura (Seneta Maalum), Judith Pareno (Seneta Maalum, ODM) na Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo.

Kampeni za za kiti hicho cha hadhi zimeshika kasi kuelekea uchaguzi utakaofanyika Jumanne juma lijalo.

Mnamo Jumanne Spika Ken Lusaka aliweka ilani kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kuondolewa kwa Profesa Kindiki ambaye pia ni Seneta wa Tharaka-Nithi kutoka wadhifa huo na akawataka maseneta wenye haja ya kuwania wachukue karatasi za uteuzi.

“Nawajulisha kwamba ilani ya gazeti rasmi imetolewa na itachapishwa leo (Jumanne). Maseneta wanaotaka kuwania nafasi hiyo wawasilishe karatasi zao za uteuzi,” Bw Lusaka akasema kwenye taarifa aliyoitoa katika kikao cha Seneti saa nane na nusu mchana.

Aliwaagiza wagombeaji kuwachukua karatasi za uteuzi kutoka kwa afisi ya Karani wa Seneti Bw Patrick Nyengenye.

Tangazo hilo lilijiri wakati ambapo kumekuwa na mazungunzo kati ya mirengo ya Jubilee na Nasa kuhusu wadhifa huo.

Kiranja wa wengi Irungu Kang’ata na mwenzake wa upande wa wachache Mutula Kilonzo Junior walisema majadiliano hayo yanaendelea lakini lengo lao ni kuzuia ushindani wa moja kwa moja kuhusu kiti hicho kati ya mirengo hiyo miwili.

“Tunapania kupata muafaka kuhusu suala hili kwa sababu kimsingi, kiti hiki ni cha Jubilee. Lakini ikiwa hawana mwaniaji anayefaa, tutawasilisha mgombeaji kwa wadhifa huo. Kile ambacho tunalenga kujiepusha nacho ni mashindano ya moja kwa moja kati yetu na wenzetu wa Jubilee,” akasema Mutula ambaye ni Seneta wa Makueni.

Kulingana na Sheria ya Seneti nambari saba, mshindi wa kiti cha Spika au Naibu Spika sharti apate angalau thuluthi mbili za kura kutoka maseneta wote 67.

Endapo hamna atakayepata idadi ya kura hitajika katika awamu ya kwanza, wagombeaji wawili wa kwanza wanatapambana katika awamu ya pili.

Mgombea atakayepata kura nyingi katika awamu hii, atatawazwa mshindi.