Omanga asema haendi popote

Omanga asema haendi popote

Na CHARLES WASONGA

SENETA maalum Millicent Omanga amepuuzilia mbali hatua ya kufurushwa kwake kutoka chama cha Jubilee akisema, “hatuendi popote.”

Kwenye ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Bi Omanga alisema alisema hajapokea barua rasmi kutoka chama hicho kuhusu kutimuliwa kwake.

Aliongeza kuwa ikiwa ni kweli kwamba amefukuzwa, basi hatua hiyo ni thibitisho ya namna wale ambao wameteka Jubilee wanavyopania kufanikisha “njama zao potovu”.

“Sijapokea barua rasmi kutoka kwa chama cha Jubilee kuhusu madai ya kufurushwa kwangu na wenzangu watano. Nimesikia habari hizo kutoka kwa vyombo vya habari. Ikiwa ni kweli, basi inatukumbusha kuhusu njama za wale ambao wameteka nyara chama hicho. Hatuendi popote!” akasema Bi Omanga.

Kulingana na barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, maseneta wengine waliofurushwa kwa “utovu na nidhamu na ukiukaji wa sera ya misimamo ya chama” ni Isaac Mwaura, Victor Prungei, Mary Seneta Yiena, Naomi Waqo Jilo na Iman Falhada Dekow.

Kulingana na Bw Tuju, sita hao walifurushwa baada ya mkutano wa Kamati ya Kitaifa Simamizi ya Jubilee (NMC) kuidhinisha ripoti ya kamati ya nidhamu iliyopata maseneta hao na hatia ya kukiuka katiba ya Jubilee na “kudharau uongozi wa chama.”

Hata hivyo, Bw Tuju alisema maseneta hao wako na nafasi ya kukata rufaa uamuzi huo ndani ya siku saba zijazo.

You can share this post!

Bamford aongoza Leeds United kuaibisha Crystal Palace...

Sonko augua akiwa rumande, alazwa hospitalini