Omanga na wenzake wapata afueni

Omanga na wenzake wapata afueni

Na CHARLES WASONGA

MASENETA sita waliotimuliwa na chama cha Jubilee wamepata afueni Jumanne baada ya Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) kusimamisha hatua hiyo hadi rufaa waliowasilisha itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mwenyekiti wa jopo hilo Desma Nungo vile vile alimzuia Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu kuondoa majina ya maseneta hao maalum kutoka orodha ya wanachama wa Jubilee.

Seneta Isaac Mwaura aliwasilisha malalamishi yake kivyake huku wenzake Millicent Omanga, Naomi Waqo, Mary Seneta, Victor Prengei na Falhada Dekow wakiwasilisha yao kwa pamoja.

“Jopo hili limesimamisha utekelezaji wa uamuzi wa Jubilee wa Februari 8 wa kuwafurusha walalamishi kutoka chama hicho, hadi maombi yao yatakaposikilizwa na kuamuliwa mbele ya wawakilishi wa pande zote,” ikasema uamuzi huo.

PPDT imeamuru kuwa kesi hiyo itatajwa mnamo Februari 16.

Mnamo Jumatatu, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alitangaza kufurushwa kuwa maseneta hao sita, uamuzi ambao alisema uliidhinishwa katika mkutano wa Kamati Simamizi ya Kitaifa (NMC) uliofanywa siku hiyo.

Hata hivyo, Katibu huyo Mkuu alisema wanasiasa hao wamepewa muda wa siku saba kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Kulingana na Bw Tuju, maseneta hao sita walifurushwa kwa kumkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta na kukaidi misimamo na maamuzi ya chama hicho tawala.

You can share this post!

Izmir Racing kurejea ulingoni katika duru ya pili ya...

Red Star Belgrade anayochezea Mkenya Richard Odada kualika...