Michezo

Omanyala aibuka wa pili mbio za Diamond League

Na GEOFFREY ANENE August 26th, 2024 1 min read

BINGWA wa Michezo ya Jumuiya ya Madola mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala amejizolea Sh767,845 baada ya kukamata nafasi ya pili kwenye duru ya 12 ya riadha za Diamond League mjini Silesia nchini Poland, Jumapili.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika ya sekunde 9.77, alitimka vizuri na kukamilisha umbali huo kwa 9.88.

Alimaliza katikati ya mshindi Fred Kerley kutoka Amerika (9.87) na Ackeem Blake kutoka Jamaica (9.89).

Bingwa wa Olimpiki 2020, Marcell Jacobs kutoka Italia aliridhika na nafasi ya nne kwa 9.93.

Mshindi na nambari tatu walituzwa Sh1.2 milioni na Sh447,910, mtawalia.

Wanawake washamiri

Nelly Chepchirchir naye alitawala mbio za 1,000m kwa dakika 2:31.24 akifuatwa na Muingereza Jemma Reekie (2:32.56), bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola mbio za 800m Mary Moraa (2:33.43) na Mganda Halimah Nakaayi (2:33.44), mtawalia.

Nyota wa Norway, Jakob Ingebrigtsen naye alivunja rekodi ya dunia ya Mkenya Daniel Komen akinyakua taji la 3,000m kwa dakika 7:17.55.

Jagina Komen alishikilia rekodi hiyo ya dunia ya umbali huo ya dakika 7:20.55 tangu 1997.

Ingebrigtsen alifuatiwa kwa karibu na Waethiopia Berihu Aregawi (7:21.28), Yomif Kejelcha (7.28.44) na Haile Telahun (7:30.97) na Mkenya Ronald Kwemoi (7:31.57) katika usanjari huo.