Omanyala apata saizi yake Ujerumani

Omanyala apata saizi yake Ujerumani

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Ferdinand Omanyala alionja kichapo chake cha kwanza mwaka 2022 katika mbio za mita 100 nchini Ujerumani, Jumatano usiku.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika ya sekunde 9.77 na muda bora duniani mwaka huu 9.85, aliduwazwa na Yupun Abeykoon kutoka Sri Lanka katika fainali ya shindano la Leichtathletik mjini Dessau.

Inspekta huyo wa polisi alilemea Abeykoon katika makundi aliposhinda mchujo wa pili kwa 10.23 naye mshikilizi huyo wa rekodi ya Sri Lanka akaandikisha 10.30.

Katika fainali, Omanyala alikamilisha umbali huo kwa 10.14 huku Abeykoon akitwaa taji kwa 10.06. Mholanzi Joris van Gool alifunga tatu-bora (10.28).

Omanyala alikuwa anatimka Ujerumani kwa mara ya kwanza naye Abeykoon alinyakua mataji ya Dessau mwaka 2020 na 2021.

Omanyala alikuwa ametawala mbio tisa mfululizo zikiwemo nne ugani Nyayo jijini Nairobi, mbili Afrika Kusini, Kip Keino Classic uwanjani Kasarani na moja nchini Italia kabla ya kupigwa breki Ujerumani.

Anaelekea mjini Ostrava kwa shindano la Golden Spike mnamo Mei 31 kabla ya kurejea nyumbani kwa maandalizi zaidi ya Riadha za Afrika zitakazofanyika Juni 8-12 nchini Mauritius.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Maombi yamedhihirisha tena unafiki wetu kama...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Uaminifu ndio upeo wa imani ya mja wa...

T L