Omanyala atangazwa mwanamichezo bora wa Septemba

Omanyala atangazwa mwanamichezo bora wa Septemba

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omurwa Omanyala ndiye mwanamichezo bora nchini mwezi Septemba wa tuzo ya LG.

Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi alinyakua tuzo hiyo ya kifahari kufuatia ufanisi wake katika duru ya mwisho ya Riadha za Dunia za Continental Tour ya Kip Keino Classic ugani Kasarani jijini Nairobi alipofuta rekodi yake ya kitaifa ya sekunde 9.86 na kuweka nyingine ya sekunde 9.77 ambayo pia ni rekodi ya Afrika.

Omanyala alikamilisha umbali huo nyuma ya Mwamerika Trayvon Bromell aliyeandikisha kasi ya juu kabisa mwaka 2021 ya sekunde 9.76. Bingwa wa zamani wa dunia na Olimpiki Justin Gatlin pia kutoka Amerika, alikamata nambari tatu kwa sekunde 10.03.

Omanyala aliyefuta rekodi ya Afrika ya raia wa Afrika Kusini Akani Simbine ya sekunde 9.84 kwenye mbio hizo za Kip Keino, alifurahia kutwaa tuzo hiyo ya LG, hasa baada ya kujumuishwa katika orodha ya wawanizi mara kadhaa bila kuishinda.

“Nafurahi kuwa mara hii nimepata kuibuka mwanamichezo bora. Ni vyema kutambuliwa nyumbani kwa kazi yako. Nashukuru kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (SJAK) kwa kuwakumbuka wanamichezo wa kiume na kike. Ni kitu cha maana sana kuwa juhudi zetu zinaonekana,” alisema Omanyala aliyeandamana na mke wake Laventer Amutavi.

Aliongeza, “Natia bidii katika mazoezi yangu, nikipiga msasa jinsi ninavyoanza mbio kwa sababu nalenga kukabiliana na majina makubwa mwaka ujao. Kuna mashindano mengi mwaka ujao ikiwemo michezo ya Jumuiya ya Madola, Riadha za Dunia, Riadha za Afrika na nina uhakika nitaandikisha muda bora.”

Naye meneja wa LG eneo la Afrika Mashariki, William Kamore, alipongeza nyota huyo akisema kuwa ni mfano hai, huku Kenya inapolenga kuwa miamba katika mbio fupi.

“Kenya imetawala mbio za kadri na ndefu kwa miaka na mikaka. Kazi ya Omanyala kwenye mbio za Kip Keino Classic bila shaka itawapa motisha kizazi kipya kujituma katika mbio za mita 100 kimataifa.”

Afisa huyo pia alitoa risala zake za rambirambi kwa familia ya malkia wa zamani wa mbio za nyika duniani Agnes Tirop ambaye alikuwa katika orodha ya wawanizi wa tuzo ya Septemba. Tirop aliuawa Oktoba 13 na kuzikwa juma lililopita.

Omanyala alizawadiwa oveni ya LG SolarDOM inayouzwa Sh65,000 sokoni ambayo ina uwezo wa kufanya kazi tatu – kuchemsha, kuchoma nyama na kuoka.

Omanyala alibwaga mwendazake Tirop aliyekuwa ameweka rekodi ya dunia mbio za kilomita 30 ya dakika 30:01 nchini Ujerumani.

Wawanizi wengine walikuwa nahodha wa timu ya taifa ya voliboli ya kinadada maarufu kama Malkia Strikers, Mercy Moim, aliyeibuka mpokeaji bora wa mpira katika Kombe la Afrika nchini Rwanda ambako Kenya ilishinda medali ya fedha.

Wanavoliboli wenzake Sharon Chepchumba aliyeshinda tuzo ya mshambuliaji bora na Gladys Ekaru aliyekuwa mzuiaji bora jijini Kigali, na mwanariadha Noah Kibet aliyeshinda mbio za mita 800 katika Kip Keino Classic kwa dakika 1:44.97, pia walikuwa katika orodha ya wawanizi.

Omanyala anaungana na washindi wengine wa tuzo hiyo ya kila mwezi ya LG ambao ni mwanatenisi Angela Okutoyi (Januari), nyota wa mpira wa vikapu Tylor Okari (Februari), bondia Elly Ajowi (Machi), bingwa wa dunia mbio za kilomita 42 Ruth Chepng’etich (Aprili), mfalme wa Milan Marathon Titus Ekiru (Mei), mshindi wa daraja ya tatu mbio za dunia za magari duru ya Safari Rally Onkar Rai (Juni), mchezaji bora wa mashindano ya mpira wa vikapu ya kinadada ya Zoni ya Tano Victoria Reynolds (Julai) na mshindi wa Riadha za Diamond League na Olimpiki mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon (Agosti).

You can share this post!

Kebs na Inable wazindua kanuni za kuwafaa walemavu...

Mbunge ataka fujo za kisiasa zichunguzwe kwa kina, akidai...

F M