Omanyala azoa laki mbili akimaliza nambari nne Riadha za Diamond League

Omanyala azoa laki mbili akimaliza nambari nne Riadha za Diamond League

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya Kenya ya mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala Omurwa alijizolea Sh220,000 baada ya kumaliza duru ya Riadha za Diamond League ya Brusseles katika nafasi ya nne nchini Ubelgiji hapo Septemba 3 usiku.

Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi, ambaye aliweka rekodi ya kitaifa ya sekunde 9.86 nchini Austria mnamo Agosti 14, alitimka umbali huo kwa sekunde 10.02 akimaliza nyuma ya Waamerika Fred Kerley (9.94), Trayvon Bromell (9.97) na Michael Norman (9.98). Nafasi tatu za kwanza ziliandamana na tuzo ya Sh1,100,000, Sh660,000 na Sh385,000, mtawalia.

“Kuandikisha sekunde 10.02 nikimaliza katika nafasi ya nne Brussels Diamond League 2021 ni kitu kikubwa, hasa kwa sababu ni fursa muhimu na baraka kushiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa. Naendelea kujifunza, kutia bidii, jitolea kwa dhati! Mambo yanaendelea kuwa mazuri! Nashukuru Mungu kwa neema yake. Asante Brussels!” alisema mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 25.

Omanyala alimaliza mbele ya Rohan Browning kutoka Australia (10.14), mshikilizi wa rekodi ya Afrika ya sekunde 9.84 Akani Simbine kutoka Afrika Kusini (10.18), Mfaransa Mouhamadou Fall (10.19) naye Arthur Cisse akavuta mkia (10.34).

Mary Moraa alikamata mkia katika mbio za mita 800 za kinadada kwa dakika 1:59.79, naye Mkenya mwenzake Edinah Jebitok akamaliza nambari 10 kati ya washiriki 14 katika mbio za maili moja ambazo Eglay Nalyanya hakukamilisha.

Bingwa wa dunia mita 5,000 Hellen Obiri alikuwa Mkenya wa kwanza katika mbio za mita 5,000 akitamatisha wa tatu na kufuatiwa na Margaret Chelimo, Lilian Kasait na Eva Cherono. Beatrice Chebet na Daisy Cherotich walimaliza nambari 11 na 14 katika kitengo hicho kilichovutia wakimbiaji 17.

Ferguson Rotich ndiye Mkenya pekee alivuna ushindi mjini Brusseles alipotawala mbio za mita 800 za wanaume kwa dakika 1:43.81. Cornelius Tuwei alimaliza mbio hizo za kuzunguka uwanja mara mbili katika nafasi ya tatu (1:45.29) kati ya washiriki 10.

Abel Kipsang na Charles Simotwo waliridhika na nafasi ya nne na tano katika mbio za mita 1,500 ambazo Boaz Kiprugut hakukamilisha. Brusseles ilikuwa duru ya 12. Jiji la Zurich nchini Uswizi litaandaa duru ya mwisho mnamo Septemba 8-9.

  • Tags

You can share this post!

Mamilioni ya fedha Henry Meja atazoa baada ya kujiunga na...

Wakili adai harudishi pesa alizotumiwa na Mungu