Omanyala, Okutoyi washauri wanatenisi chipukizi jinsi ya kufaulu

Omanyala, Okutoyi washauri wanatenisi chipukizi jinsi ya kufaulu

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Ferdinand Omanyala na Angella Okutoyi waliwapa motisha wanatenisi 120 chipukizi walio chini ya umri wa miaka 12 wakati wa makala ya kwanza ya Ferdinand Omanyala 10s katika ugani wa Nairobi Club mnamo Septemba 24, 2022.

Bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola, Omanyala, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 (sekunde 9.77), alieleza furaha kupatia kizazi hicho kipya msukumo.

“Ilikuwa hafla nzuri. Idadi ya chipukizi waliojitokeza inaridhisha sana. Watoto walikuwa wachangamfu na kumutishwa na kile nafanya katika riadha na walifurahi kuniona,” alisema Inspekta huyo wa polisi katika mahojiano.

Balozi huyo wa mradi wa tenisi ya chipukizi pia alifurahia kucheza na chipukizi hao na kuwaonyesha kuwa yeye si tofauti nao. “Wangali wadogo, lakini wanaweza kutimiza kile wanataka maishani. Niliwaeleza wasife moyo na pia wachukulie elimu kwa uzito kwa sababu ndio msingi wa vitu vizuri,” Omanyala aliambia Taifa Leo.

Omanyala alicheza mechi ya maonyesho na malkia wa tenisi Okutoyi. Kwa upande wake, bingwa wa mashindano ya Kenya Open 2018 na Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 mwaka 2021 Okutoyi alifurahia kuwapa chipukizi mawaidha. “Wana bahati kuwa kuna mtu anayeweza kuwapa ushauri kama huu. Mimi sikuupata nikiwa mdogo,” alifichua na kushukuru Omanyala kujitokeza kusaidia tenisi.

Okutoyi alishauri wachezaji wote kutia bidii ili kutimiza ndoto zao. “Natumai nitapata kuwaona siku moja wakishiriki mashindano ya haiba ya Grand Slam,” alisema. Alifichua kuwa atashiriki shindano moja nchini Tunisia na lingine Nairobi kabla ya mwaka kukamilika. Okutoyi na Omanyala pia walipata kucheza ugani Nairobi Club.

Kocha maarufu wa tenisi Veronica Osogo aliyeomba Omanyala awe balozi wa JTI, alifurahishwa na ushirikiano na mtimkaji huyo akisema amepitia mengi kufika kiwango cha juu. Katibu wa Shirikisho la Tenisi Kenya Wanjiru Mbugua kujitokeza kwa Omanyala kwenye mashindano hayo ni motisha kubwa kwani pia alisaini tishati na na vyeti vya kushiriki mashindano.

  • Tags

You can share this post!

Njaa na Ukame: Baadhi ya wakazi wa Magarini walazimika kula...

MWALIMU: Siri yake darasani iko katika nyimbo

T L