Omanyala sasa alenga dhahabu ya Riadha za Dunia 2023 na Olimpiki 2024

Omanyala sasa alenga dhahabu ya Riadha za Dunia 2023 na Olimpiki 2024

NA GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Afrika na michezo ya Jumuiya ya Madola mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala ameweka malengo makubwa ambapo anataka dhahabu kwenye Riadha za Dunia 2023 nchini Hungary na Olimpiki nchini Ufaransa 2024.

Omanyala,26, pia alifichua kuwa atashiriki riadha za Diamond League akilenga kutwaa taji katika fainali mnamo Septemba 16-17, 2023 mjini Eugene jimboni Oregon, Amerika.

Alieleza pia atakuwa na kambi ya mazoezi kwa angaa miezi mitatu nchini Italia kabla ya Riadha za Dunia mjini Budapest, Hungary mnamo Agosti 19-27 mwaka ujao.

Omanyala alisema hayo baada ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Kenya (SJAK) kumtangaza mwanamichezo bora wa mwezi Agosti. Alijishindia mashine ya kufua nguo inayogharimu Sh105,000. Omanyala, ambaye alinyakua tuzo hiyo Septemba 2021 baada ya kuandikisha rekodi mpya ya Afrika 100m ya sekunde 9.77, alipokea tuzo ya pili kwa kushinda taji la Jumuiya ya Madola mjini Birmingham, Uingereza mnamo Agosti 3, akiwa ni Mkenya wa kwanza kufanya hivyo tangu Kenya ipate uhuru mwaka 1963.

“Malengo yangu katika msimu uliokamilika yalikuwa kupata dhahabu. Nilifanikiwa kushinda Riadha za Afrika katika mita 100 na mita 100 kupokezana vijiti (4 x 100m) na kuwa bingwa wa Jumuiya ya Madola. Tulitaka kupata medali kwenye Riadha za Dunia mjini Eugene mwezi Julai, lakini kila kitu hufanyika na sababu,” alisema afisa huyo wa polisi jijini Nairobi akiandamana na mke wake Laventa Amutavi.

Omanyala anasema alipata mafunzo mwaka 2022 na kutangaza kuwa atazamia matayarisho kwa kati ya miezi mitano na sita kabla ya shindano lake la kwanza kati ya Machi na Aprili 2023.

Alifichua kuwa atapunguza idadi ya mashindano atashiriki, hasa baada ya kutimka 47 msimu 2022. Pia, Omanyala alisema atadumisha maafisa wanaofanya naye kazi.

Bingwa huyo wa Kip Keino Classic 2022 alifichua kuwa baadhi ya duru za Diamond League zilimkataa kwa sababu aliwahi kutumikia marufuku ya miezi 14 kuanzia Septemba 14 mwaka 2017 kwa kupatikana ametumia dawa iliyopigwa marufuku ya Bethamesone. “Hatuwezi kulazimisha wale wamekataa kunikubalia kushiriki mashindano yao,” alisema Omanyala akiongeza kuwa analenga kukimbia mbio nyingi kwenye Diamond League msimu ujao.

Omanyala pia alikiri kuwa alilenga kuimarisha muda wake bora katika 100m kutoka 9.77 hadi 9.6 mwaka 2022, “lakini haikuwezekana kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata jeraha la goti katikati mwa msimu”. Atalenga kuimarisha idara zote za mazoezi yake wala sio tu jinsi ya kuanza mbio na kumaliza mita 50 za mwisho.

“Kuwa bingwa wa dunia lazima uwe sawa katika idara zote kwa hivyo nitazishughulikia zote,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukikataa kubadilika ujue kuwa...

Wakazi wa Garashi wahimizwa kujenga vyoo

T L