Omanyala sasa ni Inspekta wa Polisi, atawakilisha idara hiyo kwenye riadha

Omanyala sasa ni Inspekta wa Polisi, atawakilisha idara hiyo kwenye riadha

Na AYUMBA AYODI

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala amejiunga na Idara ya Polisi (NPS) Ijumaa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mitandao ya kijamii ya idara hiyo, Omanyala, 25, amechukua majukumu mapya ya kupeperusha bendera ya Polisi katika mashindano ya riadha.

Taarifa hiyo imefichua kuwa Omanyala aliarifiwa kuhusu majukumu yake mapya Ijumaa asubuhi alipotembelea Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai katika afisi yake kwenye jumba la Jogoo House jijini Nairobi. Atatumikia idara hiyo kama Inspekta.

Afisa anayehusika na masuala ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) Johnson Kinyua na mkuu wa mawasiliano wa Chama cha Wanafunzi katika chuo hicho (UNSA) Joshua Sirma walihudhuria kikao hicho.

Omanyala ameshukuru NPS na serikali kwa kusaidia talanta na kuahidi kuwa ‘atarudisha mkono’ kwa kuvuna mafanikio uwanjani.

“Ni heshima kubwa kuhudumia Idara ya Polisi na ninaahidi kufanya vyema kama mwanariadha,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu kuwa kuna maisha baada ya uchezaji.

Mutyambai alimsihi Omanyala kudumisha nidhamu yake katika michezo ili aweze kufikia kiwango cha juu kabisa anachoweza kufika na pia kutekeleza majukumu yake mapya kama mwanariadha wa polisi.

“Nakutakia mema katika kutumikia taifa lako,” alisema Mutyambai.

Omanyala ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Digrii ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Alianza kugonga vichwa vya habari kwa matokeo mazuri aliposhiriki mashindano jijini Lagos, Nigeria alikovunja rekodi ya kitaifa kwa kutimka mbio za mita 100 kwa sekunde 10.01 mnamo Machi 30, 2021.

Muda wake ulitosha kumuingiza Olimpiki 2020, ingawa alihitaji pia kutafuta tikweti hapa nyumbani. Kwnye Olimpiki, alitimka 10.01 katika raundi ya kwanza kabla ya kuimarisha rekodi yake ya kitaifa hadi 10.00 katika nusu-fainali.

Aliingia katika historia ya Kenya kwa kuwa mtu wa kwanza kukamilisha mbio za mita 100 chini ya sekunde 10.00 aliposhinda mashindano ya Josko Laufmeeting nchini Austria kwa sekunde 9.96 katika nusu-fainali mnamo Agosti 14 kabla ya kunyakua taji kwa sekunde 9.86.

Mchezaji huyo wa zamani wa raga alishinda taji la Kip Keino Classic mnamo Septemba 18 kwa rekodi mpya ya Afrika ya 9.77 baada ya kufuta ile ya raia wa Afrika Kusini Akani Simbine ya 9.85 ugani Kasarani.

Omanyala sasa anaungana na mastaa David Rudisha, Geoffrey Kamworor, Vivian Cheruiyot, Julius Yego na Ezekiel Kemboi, miongoni mwa wengine. TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Korti yapatia serikali kibali kutwaa jumba la aliyeuawa

Wakazi wa Kiambu wahimizwa kuendea chanjo ya corona

T L