Habari Mseto

Omar Lali kujibu shtaka la mauaji

July 13th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MPENZI wa marehemu Tecra Muigai, Omar Lali sasa amepatikana na kesi ya kujibu kuhusiana na kifo cha binti huyo wa mmiliki wa kampuni ya pombe na mvinyo ya Keroche Breweries, Bi Tabitha Karanja.

Bi Tecra alifariki mnamo Mei 2, 2020, wakati akipokea matibabu ya majeraha aliyopata baada ya kuanguka kutoka kwa ngazi za nyumba ya kibinafsi aliyokuwa akiishi na Lali eneo la Shella, Kaunti ya Lamu Aprili 27.

Lali amekuwa mshukiwa mkuu kuhusiana na utata unaozingira kifo cha Bi Tecra.

Alikamatwa mnamo Mei 3, 2020, na kisha kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 mnamo Mei 27.

Katika kikao cha mahakama kilichoandaliwa kupitia mtandao wa Intaneti na kuongozwa na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba mnamo Jumatatu, Upande wa Mashtaka umeambia korti kwamba wamepata ithibati kamili ya kumshtaki Lali kwa mauaji.

Kiongozi wa Mashtaka Eddie Kadede na mwenzake, Zachariah Kiongo, wamesema walifikia uamuzi huo baada ya kuchunguza kwa makini ripoti ya upasuaji wa maiti, mawasiliano na rekodi za simu ya mshukiwa pamoja na ripoti za mashahidi.

Upande wa familia ya Bi Tecra unawakilishwa na mawakili Elisha Ongoya, Victor Soita na majaji wakuu, James Orengo na Mwaure Waihiga.

Wawakilishi hao wa familia wanasema wametosheka na upande wa mashtaka wa kumshtaki Lali kwa mauaji, wakisisitiza kuwa hatua hiyo itahakikisha haki imepatikana kwa mujibu wa sheria na wakataka na wakaitaka mahakama kumwasilisha mshukiwa mbele ya mahakama ili kujibu mashtaka hayo.

Naye wakili wa Lali, Aboubakar Yusuf, anasema licha ya kwamba hajazuia kushtakiwa kwa Lali kwa mauaji, yeye bado anaamini atathibitisha kwamba mteja wake hana hatia hata atakapowasilishwa kortini kujibu mashtaka hayo ya mauaji.

Mahakama ya Lamu kupitia Bw Temba imekubali uamuzi wa upande wa mashtaka wa kumshtaki Lali kwa mauaji, hivyo wakaamuru maafisa wa uchunguzi wa kesi hiyo kumwasilisha mshukiwa katika mahakama kuu ya mjini Garsen katika kipindi cha saa 24 zijazo ili kula kiapo kuhusiana na shataka hilo linalomkabili.

Ukuruba wa Bi Tecra na Lali – ambaye kazi yake ni kutoa huduma za watalii wanaozuru ufuo wa bahari eneo la Lamu – ulianza katikati ya mwaka 2019.

Wawili hao walikuwa wakionekana kwenye maeneo ya burudani wakijivinjari kwa vinywaji kabla ya Bi Tecra kuanguka kutoka kwa ngazi na kujeruhiwa kabla ya kifo chake baadaye.

Bi Tecra alizikwa katika hafla iliyoandaliwa nyumbani kwao mjini Naivasha.