Makala

OMAUYA: Jaji Mkuu David Maraga atakumbukwa kwa ujasiri

December 14th, 2020 2 min read

Na MAUYA OMAUYA

USIONE wembamba wa reli, garimoshi na uzito wa mabehewa yake hupitia hapo.

Huu ndio msemo mwafaka kutanguliza wasifu wa Jaji Mkuu David Kenani Maraga ambaye ameanza likizo ya kustaafu kutoka usimamizi wa Idara ya Mahakama nchini.

Wachanganuzi awali walikosea kwa kudhania Maraga atakuwa kibaraka cha wanasiasa waliokuwa mamlakani.

Aliwashangaza kwa ujasiri wake wa kutetea sheria na kukabili maadui wa haki.

Maraga atasalia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kuongoza jopo lililofutilia mbali uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto mnamo 2017, kufuatia hitilafu za matokeo ya kura za urais.

Kenya ndilo taifa la kwanza barani Afrika kutekeleza uamuzi wa aina hiyo dhidi ya kiongozi wa nchi aliye usukani.

Uamuzi wa Maraga na wenzake uliamsha kero moyoni mwa Rais Kenyatta na hakuficha ghadhabu yake dhidi ya Mahakama ya Juu na waliohusika.

Aliwafokea kwa vitisho, na kufikia kustaafu kwake Maraga na serikali ya Kenyatta wamekuwa katika mkwaruzano na kurushiana cheche za lawama.

Hivi majuzi, Jaji Mkuu alimtaka Rais kuvunja Bunge la Kitaifa kwa kushindwa kutekeleza sheria ya usawa wa jinsia.

Kwa upande wake, serikali imebana mahakama koo kwa kufinya bajeti yake huku Rais akidinda kuteua majaji waliotarajiwa.

Kitendo cha kufutilia mbali uchaguzi wa urais 2017 kiliamsha matumaini miongoni mwa wananchi na ujasiri kwa majaji nchini.

Kiliwachochea majaji wa kila kitengo kufanya maamuzi pasina kuzingatia hadhi ya mhusika katika jamii.

Hakuna kiungo muhimu katika ustawi wa demokrasia kama uhuru na uwazi wa mahakama. Hapo awali, imani katika idara hiyo ilikuwa finyu sana.

Kote barani Afrika, viongozi walio mamlakani wamekuwa wakifyeka haki za wapinzani wao na ‘wanyonge’ kwa muda mrefu.

Uamuzi wa Maraga na wenzake ulifungua ukurasa mpya kwenye mizani ya haki.

Kuna wengine kama vile wakili Ahmednassir Abdullahi wanaodai Maraga hajafaulu kurutubisha ukuaji wa sheria ipasavyo.

Abdullahi anasema Maraga ni mithili ya simba mwenda pole ambaye alivikwa taji la ukuu usiomfaa.

Hata hivyo, simba mwenda pole ndiye mla nyama. Maraga si kiongozi wa kujinadi kwa maneno; na hapendi kutanua kifua kuhusu yale ametekeleza.

Ada ya mja hunena, mwungwana ni vitendo. Kwa hakika, haki kwa umma haihitaji kusemwa bali kutendwa.

Katika bara lililogubikwa na udikteta wa kiwango cha juu, uongozi wa Maraga umeonyesha kwamba wakuu wa idara za mahakama wanaweza kuwa nguzo muhimu kuzima ukatili wa wanasiasa na kufanikisha utoaji haki kwa raia wa chini.

Tunatumai Jaji Mkuu ajaye atapaa zaidi ya Maraga.

[email protected]