Makala

OMAUYA: Utawala Tanzania uzingatie haki na demokrasia

November 16th, 2020 2 min read

Na MAUYA OMAUYA

NATANGULIZA kwa hadithi ya Mfalme Simba na wanyama wenzake ambao walitoka mawindoni na vipande vitatu vya minofu. Wote walikuwa na njaa kali.

Simba alitwaa kipande cha kwanza akatafuna kinamfaa na anastahili yeye kama mrithi wa ukoo wa kifalme, hakuna aliyepinga. Simba akatwaa kipande cha pili akasema ni chake kwa sababu ya ujasiri aliodhihirisha porini katika uwindaji wa siku hiyo. Akawaeleza, ‘bila juhudi na nguvu zangu, hatungepata chochote.’ Nani angepinga ukweli huo?.

Hatimaye Simba akawaeleza, ‘kwa hekima kuu kama kiongozi wenu nimeonelea niweke kipande cha tatu hapa ikuluni chini ya ulinzi wangu, kama akiba katika hazina kwa ajili ya vizazi vyenu na siku zijazo’… Tafakari hayo.

Mgema John Pombe Magufuli alisifiwa sana, sasa amelitia tembo maji. Hii Ni hususan baada ya kushinda kipindi cha mwisho kama Rais. Nimemweka kwenye mizani ya demokrasia na amefeli. Sawa na Mfalme Simba, Magufuli amejitwalia urais kwa kishindo, amenasa bunge lote na kudhibiti asasi za mahakama na ulinzi. Yote haya Ni katika hali iliyogubikwa na tuhuma kali za udikteta.

Ukomavu wa demokrasia unaashiriwa na jinsi taifa linawashughulikia wanyonge, makundi ya wachache, wenye maoni tofauti, wapinzani wa dola na zaidi uwepo wa uhuru wa raia kujieleza, kukosoana na hata kutofautiana katika misimamo bila hofu ya kuzimwa.

Magufuli alizoa asilimia 84 ya kura ya urais. Ifahamike kuwa katika demokrasia ya uwazi, ushindi wowote wa zaidi ya thuluthi mbili una hitilafu fulani. Hata Sadam Hussein wa Iraq alishinda uchaguzi kwa asilimia mia kwa mia mwaka wa 2002. Huo sio umaarufu, ni kejeli kwa demokrasia.

Chama chake tawala cha CCM kimezoa karibu viti vyote bungeni. Ilikuwa kawaida kwake kuwaeleza wananchi eti wakihitaji matunda ya utawala wake, yatapatikana tu kupitia mitandao ya viongozi walioteuliwa chini ya chama tawala. Kwa sababu mhitaji hana haya, raia walimiminika kwa CCM.

Ukomavu wa demokrasia haupatikani kwa wingi wa hesabu ya kura katika mazingira ambako mpinzani amelemazwa na vikwazo.

Katika ndondi au miereka itakuwa jambo la fedheha kumenyana na mshiriki aliyefungwa minyororo miguuni na mikononi, kisha akabanwa mdomo, kilio chake ni sawa na dua la kuku, halimpati mwewe. Inasikitisha zaidi kwamba sheria za Tanzania haziruhusu kupinga matokeo ya kura ya urais hata mahakamani.

Hata baada ya uchaguzi huo, viongozi na wanaharakati wanazidi kuhangaishwa na kukamatwa. Viongozi wa upinzani kama Freedman Mbowe, mwenyekiti wa CHADEMA, mbunge Godbless Lema, meya Isaya Mwita walitiwa mbaroni na kutibua jaribio la maandamano kupinga shughuli za uchaguzi wa Oktoba.

Halima Mere, kiongozi wa kina mama upinzani alikamatwa siku ya kupiga kura na kisha akapoteza kiti chake. Kinara wa chama cha ACT-Wazalendo aling’atuliwa katika eneo la Kigoma. Visiwani Zanzibar ilikuwa kichapo kutoka kwa jeshi la polisi.

Vyombo huru vya habari au vya kigeni vilinyimwa kibali na mitandao ya kijamii kuzimwa siku ya uchaguzi. Wakaguzi wa kigeni hasa ulaya hawakuruhusiwa na Ikumbukwe mikutano ya kisiasa za upinzani ilipigwa marufuku mnamo mwaka wa 2016.

Katika hali hii, hata mpinzani mkuu wa urais, Mhe Tundu Lissu ametorokea Ubelgiji kuokoa nafsi yake. Viongozi wengine wamo mafichoni Kenya. Simba Maghufuli ametwaa minofu yote. Ni masikitiko.

[email protected]