Makala

OMAUYA: Viongozi wetu wataona aibu wakiambiwa aliyofanya Sankara

October 5th, 2020 2 min read

Na MAUYA OMAUYA

Thomas Isidore Sankara alikuwa kiongozi ambaye Waafrika wote wanatakiwa kumuiga kwa jinsi ambavyo alikuwa na mawazo makuu ya ustawi wa taifa.

Alikuwa kiongozi wa Burkina Faso.

Rais Sankara alitwaa uongozi akiwa na umri wa miaka 33 akaongoza 1983 hadi 1987 alipouawa kupitia mapinduzi.

Katika utawala wake wa miaka michache, Rais Sankara hakubahatisha uongozi. Alikuwa na mambo matatu; kwanza kuondoa umaskini kote kwa taifa, pili kuhepa misaada ya kimataifa, na tatu kuepuka mikopo ya nje haswa kutoka IMF na Benki ya Dunia.

Alisimama kidete kuwa raia wake wataamua maisha yao ya baadaye. La muhimu ni kwamba Rais Sankara aliamua kuwa lazima nchi ipande miti milioni 10 kumaliza ukame wa eneo la Saher. Fikiri mawazo kama hayo yanaweza kubadili ardhi kame kaskazini mwa Kenya.

Rais Sankara aliamua kwamba kila kijiji kinahitaji zahanati katika miaka michache. Lililokuwa muhimu ni kwamba alitumia raia wenyewe kujenga kliniki hizo na chini ya miaka mitatu zaidi ya watoto milioni mbili walipokea chanjo dhidi ya maradhi yaliyokuwa yanasumbua jamii.

Falsafa yake ilienea kote kwa sababu alikuwa kiongozi wa kusema na kutenda, hakuwahi kuambia raia wafanye kile hangewaongoza wafanye wote.

Baada ya kutwaa uongozi, la kwanza alihakikisha ni viongozi wote kukataa unyonyaji wa kila aina kwa kuhakikisha wote wanaishi maisha sawa na raia. Aliuza magari yote makubwa makubwa na ya kifahari. Hakuna kiongozi aliruhusiwa kuishi maisha yanayozidi raia wake. Kwa kifupi, kiongozi hawezi kuzidi mwajiri ambaye ni raia.

Hakuna kiongozi aliruhusiwa kusafiri ng’ambo kwa raha zake kwa jina la taifa na hakuna gari la Mercedes liliruhusiwa kutumiwa na waziri wa serikali.

Nionavyo, hapa Kenya wanyonyaji tunaong’ang’ana nao wangejua hawajui. Chini ya miaka minne, Rais Sankara alijenga Shule 350 kwa taifa lake dogo na akahakikisha hakuna kwenye nchi ambako mwanamke anadhulumiwa. Mwenyewe alipiga marufuku ukeketaji wa wasichana. Serikali yake ilihakikisha kina mama wako kwenye uongozi. Mwishowe, hata wapinzani wake walisema Sankara anatetea sana kina mama.

Tafakari kwamba ni mwaka wa 2020 na nchi kama Kenya inazidi kupambana na matatizo ya kijinsia, matatizo ambayo Sankara, kijana wa miaka 33 aliona ni upuzi usiofaa. Kuna jambo kubwa zaidi ambalo Sankara aliwapa watu wake, aliwapa jina na kubadili uafrika wao, alipatia raia hadhi.

Chini ya ukoloni wa Ufaransa taifa liliitwa Upper Volta. Alipotwaa uongozi alibadili jina la nchi likawa Burkina Faso halafu akatangaza kuwa kila raia ni wa Burkinabe ambayo ina maana ya “mtu timamu” mtu asiye kombokombo, asiye na ukora wowote. Yaani Sankara na udogo wake wa umri alionyesha nchi umbali ambao viongozi wetu wameshindwa kuona baada ya karibu miaka 60? Balaa!

Mawazo ya Sankara yanazidi kushabikiwa hadi leo japo nchi ilibadilika kufuatia kuuawa kwake.

Tunahitaji Thomas Sankara hapa nchini Kenya.