Kimataifa

Ombaomba feki akamatwa jijini akijifanya hana mkono

July 11th, 2018 1 min read

Na DAILY MONITOR na VALENTINE OBARA

KAMPALA, UGANDA

POLISI wamekamata mwanamume aliyekuwa akijifanya ombaomba asiye na mkono.

Shafik Bakulu Mpagi alikamatwa na polisi wa Mini Price walioarifiwa kumhusu na rafiki yake wa karibu aliyemwona akiomba wapitanjia pesa katika kiingilio cha jengo la kibiashara la Mukwano Arcade, akiwa na mkono feki uliokatwa.

Polisi walikimbia mahali hapo wakamwagiza kutoa vitambaa alivyokuwa ametumia kufunika mkono wake.

Umati uliokuwa mahali hapo ulishangaa kuona kwamba alikuwa ni tapeli kwani mkono wake hauna kasoro yoyote.

Msemaji wa Polisi wa Kampala, Luke Owoyesigyire, alisema Mpagi amekuwa akitumia vitambaa vichafu kufunika mkono wake aliojifanya kuwa ulikatwa ili watu mahurumie na kumpa pesa.

“Kuna watu wengi ambao hujifanya ni masikini na kuja kuoma pesa barabarani sawa na jinsi Bw Mpagi amekuwa akifanya kwa hivyo wasamaria wema wako hatarini kutapeliwa,” akasema.

Msemaji huyo aliongeza kuwa idadi ya matapeli aina hiyo wamezidi kuongezeka jijini.

Aliongeza kuwa mwanamume huyo alijitetea kwamba yeye hufanya hivyo kwa kuwa hana ajira.